Shirikisho la Soka Barani Ulaya (UEFA) limetangaza kuwa Fainali za Ubingwa wa Ulaya kwa Wanawake mwaka 2029 zitafanyika nchini Ujerumani, baada ya nchi hiyo kuzishinda Poland na zabuni ya pamoja ya Denmark na Sweden katika kikao cha utendaji kilichofanyika Nyon.

Rais wa Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB), Bernd Neuendorf, alisema mashindano hayo yatakuwa kwa ajili ya kila mtu, akiwakaribisha mashabiki kutoka kote ulimwenguni kuja kushiriki katika tamasha hilo la soka la wanawake.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Ujerumani kuandaa mashindano makubwa ya soka la wanawake tangu Kombe la Dunia 2011, baada ya kushindwa jaribio la kuandaa Kombe la Dunia la 2027 lililotwaliwa na Brazil.

Ujerumani tayari imewahi kuwa mwenyeji wa fainali za Euro mwaka 1989 na 2001, na timu yake ya taifa ndiyo yenye mafanikio makubwa zaidi katika mashindano hayo ikiwa imetwaa taji mara nane.

Ujerumani 2025 | Bernd Neuendorf baada ya kuchaguliwa tena kuwa Rais wa DFB
Rais wa Shirikisho la Soka la Ujerumani (DFB), Bernd Neuendorf, alisema mashindano hayo yatakuwa kwa ajili ya kila mtu.Picha: Gerhard Schultheiß/IMAGO

Neuendorf alisema mafanikio ya kupata uenyeji yalitokana na safari ndefu na juhudi za watu wengi ndani ya DFB waliopigania pendekezo hilo, akiwashukuru wote waliounga mkono jitihada hizo.

Kipaumbele: Viwanja vikubwa, mashabiki wengi na mafanikio ya kifedha

Ujerumani inapanga kuandaa mashindano hayo katika miji minane: Cologne, Dortmund, Düsseldorf, Frankfurt, Hanover, Leipzig, Munich na Wolfsburg, ingawa Uwanja wa Olimpiki wa Berlin hautatumika kutokana na wasiwasi wa kifedha na mikataba.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Rais wa UEFA Aleksander Ceferin ilipokelewa kwa furaha kubwa na ujumbe wa Ujerumani, ambao ulihusisha kocha wa timu ya taifa Christian Wück na nahodha Giulia Gwinn, siku moja baada ya timu hiyo kupoteza 3–0 dhidi ya Hispania katika fainali ya Nations League.

Katika pendekezo lao, DFB iliweka mkazo kwa uwezo wa kujaza viwanja na kuongeza mapato, ikilenga kuvutia angalau mashabiki milioni moja viwanjani—hatua inayotarajiwa kuondoa changamoto za kiuchumi ambazo hapo awali zimekwamisha wenyeji wa mashindano ya wanawake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *