Yemen imegundua utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, ikiwa ni pamoja na akiba kubwa ya dhahabu, chuma, titani na madini ya viwandani. Rasilimali hizi zinaweza kufungua njia ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha nafasi ya kimkakati ya Yemen katika eneo hili zima.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars; mbali na Yemen kuwa katika eneo muhimu la kiistratijia na kimkakati katika Bahari Nyekundu hususan kutokana na kuwa kwake na Lango Bahari la Bab al-Mandab ambayo ni moja ya njia muhimu zaidi za baharini duniani, nchi hiyo ya Kiarabu ina utajiri mkubwa pia wa rasilimali. Mbali na kuziunganisha Bahari Nyekundu na Bahari ya Hindi, Yemen iko kwenye njia muhimu mno ya biashara ya kimataifa, hasa usafirishaji wa mafuta na bidhaa kati ya mabara ya Asia, Afrika na Ulaya. Lakini si hayo tu, ndani ya ardhi ya Yemen pia, Mwenyezi Mungu ameineemesha ardhi hiyo kwa utajiri mkubwa wa maliasili yakiwemo madini muhimu na ya kila namna.
Njama za kutaka kuidhibiti Yemen zimeongezeka hasa kutokana na msimamo wa serikali ya San’an wa kuwa pamoja na ndugu zao wa Palestina. Wakati wa vita vya Ghaza, Yemen ilifunga njia ya baharini na kushambulia meli na vyombo vyote vilivyokuwa vinatumia eneo lake kuelekea kwa utawala wa Kizayuni, suala ambalo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni na ni moja ya masuala yaliyochangia mno kuilazimika Israel na Marekani kukomesha vita vya Ghaza. Lakini kama tulivyoashiria hapo juu, umuhimu wa Yemen hauishii tu kuwa kwake katika eneo la kimkakati, bali nchi hiyo ina akiba kubwa pia ya madini ya kila namna na muhimu sana duniani.
Migodi ya dhahabu na fedha ni miongoni mwa rasilimali muhimu zaidi za madini nchini Yemen, huku maeneo 50 yakifanyiwa utafiti hivi sasa kwa ajili ya kugundua utajiri mwingine wa asili wa nchi hiyo. Kwa mujibu wa duru za kuaminika zilizotoa ripoti yao mwaka 2013, utajiri wa madini ya dhahabu nchini Yemen ulikadiriwa kuwa ni takriban tani milioni 100, ambazo nyingi ziligundiliwa katika majimbo ya Hadhramaut na Hajjah. Hapa tutaorodhesha baadhi ya migodi hiyo:
Migodi ya dhahabu:
Mgodi wa Wadi Madan:
Mgodi wa Wadi Madan, uliogunduliwa mwaka wa 1967 katika Mkoa wa Hadhramaut, kaskazini magharibi mwa mji wa Mukalla mji ambao hivi sasa uko chini ya udhibiti wa wavamizi wanaoungwa mkono na muungano wa Saudi Arabia na Imarati, ni moja ya migodi ya dhahabu ya zamani na muhimu zaidi nchini Yemen.
Takwimu zinaonesha kuwa mgodi huo una takriban tani 678,000 za miamba yenye mkusanyiko wa takriban tani 10 za dhahabu.

Mgodi wa Al-Haraqa:
Mgodi wa Al-Haraqa upo Aflah Al-Sham katika Mkoa wa Hajjah ambao uko chini ya udhibiti wa Serikali ya Wananchi wa Yemen, karibu na mpaka wa Saudi Arabia. Huo ni moja ya migodi mikubwa zaidi ya dhahabu nchini Yemen. Mgodi wa Al-Haraqa uligunduliwa mwaka wa 1996 na kampuni ya Kantex ya Canada.
Uchunguzi wa kampuni ya Kantex uligundua kwamba kuna zaidi ya tani 96 za dhahabu katika mgodi huo. Kwa mujibu wa Utafiti wa Jiolojia wa Yemen, akiba ya dhahabu ya eneo la Al-Haraqa inakadiriwa kuwa ni takriban tani milioni 31.6 za madini ya dhahabu pekee. Kiujumla ni kwamba dhahabu inayopatikana katika mgodi huo mmoja tu inaweza kukadiriwa kuwa ni kati ya tani milioni 31 hadi 52.
Migodi ya Risasi na Zinki:
Mgodi wa Jabal Şalab:
Mgodi wa Jabal Şalab ulioko katika Mkoa wa Sana’a wenye akiba ya madini ya risasi na zinki ni moja ya migodi mitano muhimu zaidi nchini Yemen. Akiba ya mgodi huu inakadiriwa kuwa ni takriban tani milioni 12.6 za madini, ambayo yana asilimia 8.86 ya zinki, asilimia 1.16 ya risasi na elementi nyingine kwa kila tani ya madini.
Madini ya Chuma na Titanium:
Migodi ya eneo la Makiras:
Mkoa wa Al-Bayda, ambao uko chini ya udhibiti wa Serikali ya Wananchi wa Yemeni, ni moja ya maeneo tajiri zaidi nchini Yemeni kwa upande wa akiba ya chuma na titanium. Eneo la Makiras lina takriban tani milioni 130 za madini ya chuma na tani milioni 46 za oksidi ya titanium. Mikoa ya Al-Rayya na Sabah pia ina miamba yenye mkusanyiko wa hadi asilimia 74 ya oksidi ya chuma.
Madini ya Viwandani:
Migodi ya Jasi na Chumvi ya Mawe:
Yemen pia ina akiba kubwa ya madini ya viwandani, ikiwa ni pamoja na utajiri mkubwa wa jasi huko Hadramaut na Al-Mahra maeneo ambayo yanadhibitiwa na vibaraka wa Saudi Arabia na Muungano wa Falme za Kiarabu yaani Imarati. Inakadiriwa kuwa maeneo hayo yana zaidi ya tani milioni 12 za madini hayo ya viwandani. Pia kuna takriban mita za ujazo milioni 337 za chumvi ya mawe katika jimbo la Al-Hodeidah, ambalo liko chini ya udhibiti wa Serikali ya Wananchi wa Yemen.
Kiujumla ni kwamba madini yana jukumu muhimu katika uchumi wa dunia. Viwanda kama vile vya kuzalisha chuma, saruji, petrokemikali, magari, na hata teknolojia mpya za kielektroniki, haviwezi kustawi bila ya kupatikana rasilimali za madini kama hayo.
Bila ya shaka ni kwa sababu hiyo ndio maana Yemen imevamiwa na kutumbukizwa kwenye vita ili kuporwa utajiri wake huo mkubwa. Migodi tuliyoitaja kwenye uchambuzi huu ni sehemu ndogo tu ya utajiri wa madini wa Yemen ambayo kama utulivu utaimarishwa na utajiri wake kutumika kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake, nchi hiyo kamwe haiwezi kuitwa maskini na wala wananchi wake wake hawawezi kuishi katika umaskini.
Lakini Yemen imetumbukizwa kwenye vita vinavyoongozwa na muungano wa Saudia na Imarati kwa usaidizi kamili wa Marekani na utawala wa Kizayuni na matokeo yake ni kwamba si tu usalama wa nchi hiyo umehatarishwa, lakini pia fursa za kutumiwa vizuri rasilimali zake zimevurugwa huku uporaji wa maliasili hizo ukiendelea katika maeneo yanayodhibitiwa na madola vamizi yenye baraka kamili za dola la kibeberu la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.