Benki ya Dunia imesema, pengo kati ya gharama za nchi maskini kulipa madeni na ufadhili mpya limefikia kiwango cha juu zaidi kwa zaidi ya miaka 50.

Benki hiyo imesema pengo hilo ni takriban dola bilioni 741 kati ya mwaka 2022 na 2024.

Benki hiyo ya Dunia imeshauri nchi kutumia mbinu rahisi za kifedha ili kurekebisha hali hiyo. 

Kwenye ripoti yake ya kila mwaka kuhusu madeni, Benki ya Dunia yenye makao yake makuu mjini Washington Marekani, imesema malipo ya riba yalipanda zaidi na kuweka rekodi mpya ya dola bilioni 415.4 mwaka 2024, licha ya nafuu ndogo iliyotokana na kushushwa kwa viwango vya riba duniani.

Masoko yanayoibukia yanageukia madeni ya ndani, hatari ya kuzuia mikopo ya benki za ndani

Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia, Indermit Gill, ametahadharisha kwamba hali inaweza kuwa inaboreka, lakini nchi zinazoendelea bado haziko salama. Malimbikizi ya madeni yanaendelea, wakati mwingine kwa njia mpya na hatari.

Benki ya Dunia yasema malipo ya riba yafikia rekodi ya dola bilioni 415.4 mwaka 2024
Benki ya Dunia yasema malipo ya riba yafikia rekodi ya dola bilioni 415.4 mwaka 2024Picha: Erwin Wodicka/Pond5 Images/IMAGO

Masoko ya dhamana yalifungua milango tena baada ya mzunguko mrefu wa kuongezwa kwa viwango vya riba. Lakini gharama ni kubwa. Riba za madeni ya dhamana zikikaribia asilimia 10, hiyo ikiwa ni mara mbili zaidi ya kabla ya mwaka 2020.

Na kwa sababu ufadhili wa gharama nafuu unazidi kupungua, nchi nyingi zimegeukia mikopo ya ndani. Mwaka jana, katika nchi 50, madeni ya ndani yaliongezeka kwa kasi kuliko madeni ya nje.

Utoaji wa mikopo wapungua kwa 76%; walazimisha ufadhili wa gharama kubwa zaidi

Benki ya Dunia inasema hii ni ishara ya ukuaji wa mashirika na taasisi za mikopo ya ndani. Lakini imetahadharisha kuwa inaweza kubana mikopo ya benki kwa sekta binafsi na kuongeza gharama za kulipia madeni kutokana na muda mfupi wa ukomavu.

Mnamo mwaka 2024, mataifa yanayoinukia yalifanyia marekebisho takriban dola bilioni 90 za madeni ya nje, kwa kiasi cha juu zaidi ndani ya miaka 14. Miongoni mwa nchi hizo ni pamoja na Ghana, Zambia, Sri Lanka, Ukraine, Ethiopia, na vilevile msamaha wa madeni kwa Haiti na Somalia.

Watunga sera katika mataifa yanayoinukia washauriwa kurekebisha bajeti zao, badala ya kukimbilia tena madeni ya nje.
Watunga sera katika mataifa yanayoinukia washauriwa kurekebisha bajeti zao, badala ya kukimbilia tena madeni ya nje.Picha: Andreas Mallinckrodt/Zoonar/picture alliance

Wakati huohuo, mikopo ya pande mbili imeshuka kwa asilimia 76 hadi dola bilioni 4.5, hiyo ikiwa ni kiwango cha chini kabisa tangu mgogoro wa kifedha wa mwaka 2008. Hali hiyo ililazimisha nchi nyingi kutegemea ufadhili wa kibinafsi wenye gharama kubwa.

Japo mikopo iliongezeka kutoka taasisi mbalimbali huku Benki ya Dunia ikitoa kiwango cha juu zaidi cha dola bilioni 36, asilimia 54 ya nchi zenye mapato ya chini ziko kwenye hatari kubwa ya madeni.

Gill ametoa ushauri kwa watunga sera katika mataifa husika kuwahi udongo ungali maji ili kurekebisha bajeti zao, badala ya kukimbilia tena madeni ya nje.

(RTRE)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *