Mazoezi maalumu ya kupambana na ugaidi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO), “Sahand 2025,” yanafanyika katika Kaunti ya Shabestar, Mkoa wa Azerbaijan Mashariki, nchini Iran.
Maoezi maalumu ya kupambana na ugaidi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai yalianza Jumatatu, Desemba 1, kwa uwenyeji wa Kikosi cha Jeshi la Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) katika Mkoa wa Azerbaijan Mashariki na yataendelea hadi tarehe 14 mwezi huu.
Katika maneva hayo ya pamoja ya kijeshi, vikosi vya majeshi ya nchi zinazoshiriki vitapitia hatua mbalimbali za mafunzo maalumu katika uwanja wa kupambana na ugaidi. Mazoezi ya “Sahand 2025” yameandaliwa na Kikosi cha Mitambo cha Imam Zaman (A.S.), mojawapo ya vitengo vya operesheni na vyenye nguvu kubwa ya jeshi la nchi kavu la IRGC. Mazoezi haya ni sehemu ya mchakato wa kila mwaka wa mazoezi ya pamoja miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai, ambayo yanalenga kuimarisha kiwango cha uratibu, kukuza ushirikiano wa ulinzi, na kuzidisha utayarifu wa kukabiliana na vitisho vya kigaidi.
Kanali wa IRGC, Shahram Askarian, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Umma wa Vikosi vya Nchi kavu vya IRGC, amesema: “Mazoezi ya Sahand 2025 yana umuhimu maalumu wa kimkakati.” Kanali Shahram Askarian ameashiria rekodi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kupambana na ugaidi na kusema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa kitovu cha mapambano dhidi ya ugaidi na makundi ya kigaidi, na zaidi ya watu 17,000 wa nchi yetu, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa shahidi na magaidi.”
Russia, Uchina, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Uzbekistan, India, Iran, na Pakistan ndio wanachama wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai (SCO).
Mazoezi ya kijeshi ya kupambana na ugaidi ya “Sahand 2025”, ambayo yanafanyika nchini Iran kwa ushiriki wa vikosi vya majeshi ya nchi wanachama, yana majukumu kadhaa muhimu katika uwanja wa kupambana na ugaidi. Mazoezi haya yanaviruhusu vikosi kutoka nchi wanachama kufanya mazoezi ya mbinu, taktiki na viwango vya pamoja katika kukabiliana na vitisho vya kigaidi.

Kwa kuzingatia utofauti wa kitamaduni na kijeshi wa wanachama, mazoezi haya ya pamoja yanasaidia kukuza taratibu na mbinu za ushirikiano katika shughuli za kupambana na ugaidi. Wakati huo huo, ushirikiano wa kijeshi na kiusalama miongoni mwa wanachama huongeza uaminifu wa kisiasa na usalama na kufungua njia ya ushirikiano mpana katika maeneo mengine.
Kutokana na eneo lake la kijiografia na uzoefu mkubwa katika kupambana na makundi ya kigaidi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi na mchango muhimu katika mazoezi haya.
Kufanyikka mazoezi ya “Sahand 2025” kunapata umuhimu mkubwa zaidi kwa kutilia maanani kwamba ugaidi ni tishio la kimataifa na unaweza kudhibitiwa tu kupitia ushirikiano wa pande nyingi. Mazoezi haya ya pamoja yanahakikisha usalama wa pamoja wa wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai dhidi ya vitisho vya kigaidi na itikadi kali, na vilevile, yanatuma ujumbe wa wazi wa kisiasa wa umoja na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama dhidi ya vitisho vya kimataifa. Sahand 2025 pia sio mazoezi ya pamoja ya kijeshi tu, bali pia ni ishara ya ushirikiano wa kiusalama wa kikanda ndani ya mfumo wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.
Kwa kuandaa na kushiriki kikamilifu katika mazoezi ya Sahand 2025, Iran inathibitisha tena nafasi na mchango wake wenye taathira kubwa katika kulinda usalama wa kikanda na kupanua ushirikiano wa kupambana na ugaidi.
Mazoezi haya na mpango wa ushirikiano wa kupambana na ugaidi wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai vinatuma ujumbe wazi wa umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama dhidi ya vitisho vya pamoja, na Iran, kwa kuchukua jukumu muhimu, inaweka msimamo wake kama moja ya nguzo kuu za usalama wa kikanda.