Katika ziara yake ya siku tatu nchini China, Macron amesema mataifa hayo mawili yanapaswa kushirikiana ili kupata amani na utulivu duniani hasa Ukraine na maeneo mengine yaliyoathiriwa na vita. Kiongozi huyo wa Ufaransa ameyasema hayo wakati ambapo anafanya juhudi za kuishirikisha Beijing katika kuishinikiza Urusi ifanye makubaliano ya kusitisha vita na Ukraine.
Akizungumza katika ukumbi wa Great Hall of the People mjini Beijing wakati wa mkutano huo kuhusu suala la Ukraine Macron amesisitiza kuwa, ” Ninatumaini kuwa China itajiunga na juhudi zetu za kupata makubaliano ya amani haraka iwezekanavyo kwa mfumo wa kuzuia mashambulizi yanayolenga miundombinu muhimu. Hili ni muhimu hasa katika majira ya baridi kali yajayo kwa kuzingatia kuwa miundombinu ya kiraia hasa nishati bado inashambuliwa na Urusi. Lakini zaidi tuna matumaini ya kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kupata amani ya kudumu inayoheshimu sheria za kimataifa”
Kwa upande wake Rais wa China Xi Jinping amesisitiza kuwa China inajitahidi kutafuta amani na ina matumaini kuwa pande mbili zinazohusika na mzozo wa Ukraine zitapata amani ya kudumu kwa njia ya mazungumzo.
Amesema Ufaransa na Beijing ambazo ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama, zinapaswa kuonesha ushirikiano wa kweli unaozingatia sheria za kimataifa, kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika utatuzi wa mizozo.
China iko tayari kufanya kazi na Ufaransa
Kuhusu ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili, Xi amesema China iko tayari kufanyakazi na Ufaransa kwa maslahi mapana ya raia wao na jumuiya ya kimataifa.
Aidha ameongeza pia kuwa Macron amekubali kufanya juhudi zaidi za kukuza ushirikiano wa kiuchumi kupitia uwekezaji na mazingira yasiyo na ubaguzi kati ya nchi hizo.
Kauli ya Xi imetolewa wakati Wizara ya biashara ya China ikiarifu kuwa biashara kati ya mataifa hayo imekua kwa asilimia 4.1 mwaka hadi mwaka na kufikia dola bilioni 68.8 za Kimarekani kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu.
Viongozi hao wawili wametiliana saini mikataba 12 ya ushirikiano baada ya mazungumzo hayo. Mikataba hiyo inajumuisha masuala ya idadi ya watu, nishati ya nyuklia na uhifadhi wa wanyama aina ya Panda.