
Akizungumza Alhamisi katika mkutano wao mjini Beijing, Macron alisema anatarajia China iunge mkono juhudi za kufikia makubaliano ya haraka ya kusitisha mashambulizi yanayolenga miundombinu ya kiraia.
“Hili ni muhimu kwa majira yanayokuja ya baridi, kwa kuzingatia kwamba miundombinu ya kiraia, hasa nishati bado inashambuliwa na Urusi. Lakini kwa upana zaidi, tuna matumaini ya kufanya kazi pamoja kwa ajili ya kupatikana amani ya haki na kudumu, ambayo inaheshimu sheria za kimataifa,” alifafanua Macron.
Kwa upande wake, Xi alisema kwamba yeye na Macron wamekubaliana kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kuongeza uwekezaji wa pande mbili na kuhakikisha mazingira yasiyo ya kibaguzi kwa biashara katika nchi zote mbili.
Pia alisisitiza umuhimu wa kusitishwa kwa uhasama nchini Ukraine, akisema China inaunga mkono juhudi zote za kupatikana kwa amani na ina matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano ya kudumu yanayokubalika na pande husika.