Kesi hiyo, chimbuko lake ni mashitaka ya mwaka 2022, imezua maswali kuhusu ni kwa nini imefufuliwa wakati huu.
Shauri hilo la jinai namba 000021172/2025, lililofunguliwa na Jamhuri tarehe 28 Agosti 2025, linadai kuwa kati ya Machi 1 na Machi 31, 2022, katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Mange alijipatia Sh138.5 milioni akifahamu kuwa ni fedha za uhalifu. Inadaiwa pia alipata fedha hizo kupitia kazi ya uandishi wa habari bila kibali na kwa vitisho. Mashitaka hayo yanatokana na kifungu 12(1)(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha, Sura ya 423 ya mwaka 2019, kwa mujibu wa Sheria ya Uhujumu Uchumi
Desemba 4, 2025, shauri hilo liliitwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hassan Makube. Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama kuahirisha kesi kwa maelezo kuwa upelelezi bado haujakamilika. Kwa upande wa utetezi, Mange hakuwa na wakili, hivyo Hakimu Makube aliutaka upande wa Jamhuri kuhakikisha taratibu zote zimekamilika ili kesi ianze kusikilizwa katika tarehe itakayopangwa.
Kesi dhidi ya Mange yaibua maswali
Kesi hii imeibua maswali kuhusu uwezekano wa Tanzania kumrejesha Mange kutoka Marekani ili akabiliwe na mashitaka.
Sheria ya Urejeshaji Watuhumiwa Kutoka Nje (Extradition Act, 2019) inalitaja kosa la utakatishaji fedha kama moja ya makosa yanayoweza kuombewa mtuhumiwa kurejeshwa nchini.
Kampeni za mtandaoni ndizo zilimuibua Mange
Mange Kimambi amekuwa mkosoaji wa serikali ya Tanzania tangu enzi za Rais Hayati John Magufuli (2015–2021), akimshutumu kwa ukiukaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa upinzani. Vilevile amekuwa mkosoaji wa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mapema mwaka huu, Mange alianza kampeni za mtandaoni za kuhamasisha maandamano ya kudai mabadiliko, akidai kuwepo kwa upotoshaji katika mchakato wa uchaguzi na akiwataka wananchi kuchukua hatua za amani kupinga matokeo. Alijitambulisha kama chanzo mbadala cha taarifa, akichapisha madai ya udanganyifu na kuendeleza ukosoaji wa mifumo rasmi.
Mtandao wa Instagram umekuwa nyenzo yake muhimu ya kuhabarisha, kuhamasisha, kuhifadhi ushahidi na kupinga simulizi za serikali na vyombo vya habari. Na sasa, serikali ya Tanzania imeamua kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanaharakati huyo.