
Marekani imesema inapitia upya uhusiano wake na Tanzania wakati kukiwa na wasiwasi kuhusu ukandamizaji dhidi ya uhuru wa kidini, uhuru wa kujieleza, vikwazo vya uwekezaji wa Marekani pamoja na ghasia dhidi ya raia.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Alhamisi imetoa tahadhari za usalama kwa Wamarekani wanaoishi Tanzania baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, kukumbwa na ghasia zilizosababishwa na maandamano.
Mamia ya watu wadaiwa kuuawa
Makundi ya kutetea haki za binaadamu, vyama vya upinzani na Umoja wa Mataifa vimesema inasadikiwa mamia ya watu waliuawa katika vurugu hizo.
Hata hivyo, serikali ya Tanzania imekanusha takwimu hizo, ikisema zimeongezwa.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na ameahidi kuchunguza vurugu hizo, baada ya machafuko hayo kusababisha mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa nchini humo katika miongo kadhaa.