Muungano wa makundi ya kisheria umeonya shirika la Microsoft kwamba utoaji wake wa huduma kwa Israel wakati wa vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza huenda ukaiweka kampuni hii kubwa ya teknolojia ya Marekani kushtakiwa katika mahakama za kimataifa.

Muungano huo unaojumuisha mashirika ya Kituo cha Sheria cha Wanaopinga Utumwa, Taasisi ya Avaaz, Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Ulaya, Kituo cha Utafiti wa Kampuni za Kimataifa (SOMO),  Kituo cha Haki za Kikatiba, Ekō, na Mtandao wa Kimataifa wa Hatua za Kisheria (GLAN).

Katika barua muungano huo umeialilaumu Microsoft kwa kusaidia, kuchochea, na kuchangia katika kutekelezwa kwa uhalifu wa ukatili na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Walieleza kuwa shirika la Microsoft limetoa huduma kwa utawala wa Israel ikiwa ni pamoja na teknolojia ya wingu, akili mnemba, na usindikaji wa data. Huduma hizo zilitumiwa katika jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Barua hiyo imesema: “Kuna msingi wa kimantiki na wa kuaminika kuamini kuwa Microsoft, kupitia utoaji wake wa teknolojia na huduma kwa jeshi la Israel, limehusika moja kwa moja katika kutekeleza uhalifu mkubwa dhidi ya Wapalestina wa Gaza, ikiwa ni pamoja na, lakini si tu, mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita, na uhalifu dhidi ya ubinadamu,” ilisoma sehemu ya barua hiyo.

Makundi hayo ya kisheria pia yalisema kuwa vyanzo vya ndani ya Israel vimeithibitishia kuwa jeshi la utawala wa Tel Aviv linategemea bidhaa za Microsoft kuchambua na kuendeleza “malengo ya mauaji” huko Gaza, pamoja na kupeleleza Wapalestina.

Israel imesababisha vifo vya angalau Wapalestina 70,117, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, tangu Oktoba 7, 2023, wakati ilipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.

Israel ililazimika kukubali kusitisha mapigano huko Gaza, ambayo ilianza kutekelezwa Oktoba 10, 2025, lakini tangu wakati huo imekiuka mapatano hayo kwa mashambulizi ya karibu kila siku dhidi ya eneo liliozingirwa la Palestina.

Zaidi ya hayo, katika barua yao, makundi hayo walisema kuwa baada ya kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Israel, Microsoft bado ni mtoa huduma mkubwa wa huduma kwa jeshi la utawala huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *