Kufuatia msukumo wa hivi karibuni wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kumaliza vita nchini Ukraine huenda Ulaya ikalazimika kukubaliana na hatua za kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Washington na Moscow, ambayo serikali nyingi za Ulaya na NATO yenyewe zinasema ndiyo tishio kubwa zaidi kwa usalama wa Ulaya.
Ingawa Waukraine na Ulaya walipinga baadhi ya vipengele vya mpango wa Marekani wa kumaliza mapigano ulioonekana kuipandelea Urusi. Hata hivyo Ulaya bado inaonekana haina nguvu sana ya kubadilisha makubaliano hayo.
Luuk van Middelaar, mkurugenzi mwanzilishi wa taasisi ya utafiti ya masuala ya siasa za kimataifa, Brussels Institute for Geopolitics, anasema: “Trump anaonekana wazi kutaka makubaliano, lakini kinachoitia wasiwasi Ulaya ni kwamba anataka makubaliano kulingana na hoja kwamba wao ni Marekani na wale ni Urusi, kwa hiyo hao wawili ni mataifa makubwa.”
Rubio ataka kuihakikishia Ulaya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema Ulaya itashirikishwa katika majadiliano kuhusu nafasi ya NATO na Umoja wa Ulaya katika makubaliano yoyote ya amani.
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius alionyesha wasiwasi wiki iliyopita akisema kwamba Ulaya haijui tena “ni miungano ipi ambayo bado inaweza kuiaminika na kudumu katika siku zijazo.”
Lakini wanadiplomasia wa Ulaya wanasema kwamba karibu kila kipengele cha makubaliano hayo kitaiathiri Ulaya — kuanzia uwezekano wa Ukraine kuachilia maeneo hadi ushirikiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Urusi.
Wasiwasi waongezeka Ulaya, kulikoni?
Lakini mpango wa Rubio wa kuukosa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa NATO unaoendelea Brussels wiki hii unaweza tu kuongezea wasiwasi wa Ulaya.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul alisema wiki iliyopita kwamba “vyombo vyao vya ujasusi vinawaambia kwa msisitizo kwamba Urusi haijafuta uwezekano wa kuanzisha vita dhidi ya NATO kabla ya mwaka 2029.”
Kauli sawia imetolewa na Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, aliyewaambia waandishi wa habari Jumatatu kwamba “Iwapo jeshi la Urusi ni kubwa, ikiwa bajeti yao ya kijeshi ni kubwa kama ilivyo sasa, watataka kulitumia tena.”
Aidha, Trump na maafisa wengine wa Marekani wameweka wazi kuwa wanaona fursa kubwa za biashara na Moscow pindi vita vitakapomalizika.
Ulaya ina karata muhimu ya majadiliano kupitia mali za Urusi zilizozuiliwa. Lakini viongozi wa Ulaya hadi sasa bado hawajafikia makubaliano juu ya pendekezo la kutumia mali hizo ili kuendelea kuisaidia Ukraine katika vita vyake dhidi ya Urusi angalau kwa miaka miwili ijayo.