Kumekuwa na kauli mbalimbali kutoka kwa viongozi wa juu wa Serikali ya Tanzania, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, wakikemea maandamano hayo yanayodaiwa kuanza tarehe 9 Desemba. Rais Samia amesisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama viko tayari kukabiliana na vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani, kauli aliyoitoa hivi karibuni alipokutana na wazee jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Rais imefuatiwa na tamko la Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime, ambaye amesema jeshi limekuwa likifuatilia taarifa mbalimbali mtandaoni kuhusu maandamano hayo. Misime anadai kuwa baadhi ya watu wanahamasishwa kufanya vitendo vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

“Mtu yoyote aliyewasikiliza na akiendelea kuwasikiliza, wanahamasishana kufanya mambo yafuatayo: Siku hiyo ya maandamano yasiyo na kikomo, maana yake tarehe 9, Disemba 2025, wanalekezana ambaye hajui kutumia silaha na hajapitia mafunzo, siku hiyo asishike silaha, wawaachie waliopata mafunzo ya kutumia silaha, kwa maana rahisi, watu hawa wanazo silaha za kutimiza lengo lao walilokusudia.” 

Tanzania l Kukatika kwa huduma za Instagram, Facebook na WhatsApp
Mkazi wa Dar es Salaam, Tanzania akijaribu bila mafanikio kufungua mtandao wa Instagram wakati huduma ya mitandao ilipokatika.Picha: Eric Boniphace/DW

Amesema pia kuwa kupitia mitandao ya kijamii kumekuwepo na wito fulani wa kuisimamisha nchi kuanzia Desemba 9, madai ambayo yameibua mjadala mpana miongoni mwa wananchi kuhusu kinachoweza kutokea siku hiyo, hususan kutokana na kumbukumbu ya matukio ya Oktoba 29.

Hofu yatanda

George Kasela, mkazi wa Mabatini jijini Mwanza, anaeleza hofu yake, akisema “Mpaka sasa tunavyoongea ndugu mtangazaji maisha ni magumu na ukizingatia mwanzo Oktoba 29 mandamano yalitokea watanzania tukakaa ndani takribani wiki nzima, maisha yalikuwa ni magumu, usafiri ulikuwa wa shida, vyakula tulikuwa hatupati kwa wakati, kwahiyo mimi nadhani maisha yatazidi kuwa magumu na kama unavyojua maisha ya mtanzania lazima atoke, arudi nyumbani ndio familia ipate chakula.”

Wakati huo huo, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wamesema kuwa kama kweli kuna madai ya kuhamasisha matumizi ya silaha— jambo ambalo halijathibitishwa wazi — basi maandamano hayo yanakosa uhalali.

“Kwa tamko la polisi kwamba wana taarifa tayari kutoka kwenye mitandao kwamba watu watakuwa na silaha, hayo sio mandamano tena inaungana pengine na mazungumzo ya Rais,” alisema.

Taarifa hizi zinakuja wakati Rais Samia akiwa tayari ameunda tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29 huku baadhi ya makundi, ikiwemo vyama vya siasa na wanaharakati yakieleza kutoridhishwa na tume hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *