Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi wanatarajiwa kuthibitisha tena ahadi yao kwa mkataba wa ujumuishaji wa kiuchumi waliokubaliana mwezi uliopita, pamoja na mkataba wa amani uliofadhiliwa na Marekani na kufikiwa mwezi Juni, ambao hata hivyo bado haujatekelezwa.

Wachambuzi wanasema diplomasia ya Marekani imefanikisha kupunguza kasi ya mapigano mashariki mwa Congo, lakini haijatatua masuala ya msingi.

Mapema mwaka huu, waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda waliteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Congo kwa mashambulizi ya haraka, hatua iliyozidisha hofu ya kuzuka kwa vita pana zaidi.

Trump atafuta sifa za kidiplomasia kwa juhudi za amani

Trump, ambaye tangu kuingia madarakani Januari amejitokeza kujaribu kuimarisha rekodi yake ya kidiplomasia, amekuwa akijihusisha katika migogoro mbalimbali kuanzia Mashariki ya Kati hadi Ukraine. Jina lake limeongezwa kwenye bango nje ya Taasisi ya Amani ya Marekani, ambako makubaliano hayo yanatarajiwa kusainiwa.

Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo huenda kusiwe na athari za haraka kwa mgogoro wa kibinadamu unaoendelea. Siku ya Jumanne, jeshi la Congo na waasi wa M23 walishutumiana kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano. Jumatano, msemaji wa serikali ya Congo, Patrick Muyaya, alilaumu M23 kwa mashambulizi ya hivi karibuni Mashariki mwa Congo, akisema yanathibitisha Rwanda “kutotaka amaniā€.

M23 halitarajiwi kuhudhuria mkutano huo na si sehemu ya makubaliano yoyote ya Congo na Rwanda.

Kongo, Rwanda bado hazijatekeleza mpango wa Trump wa Juni

Chini ya mkataba unaoungwa mkono na Marekani, Congo inatakiwa kuchukua hatua dhidi ya kundi la waasi la FDLR, linalopinga M23, huku Rwanda ikitakiwa kuondoa majeshi yake ndani ya Congo. Hata hivyo, hakuna maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kutekeleza masharti hayo tangu mwezi Juni.

Washington D.C. Marekani 2025 | Donald Trump na wajumbe wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
Kongo, Rwanda bado hazijatekeleza mpango wa Trump wa JuniPicha: Andrew Caballero-Reynolds/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, wana matumaini kwamba baada ya kutiwa saini, kutakuwa na mabadiliko chanya katika uwanja wa vita.

Rwanda imekuwa ikikanusha kuiunga mkono M23 na inadai kwamba vikosi vyake hufanya operesheni za kujilinda dhidi ya wanamgambo wa kihutu wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya 1994. Hata hivyo, ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ya mwezi Julai ilisema Rwanda inaongoza na kudhibiti harakati za M23.

Kwa upande mwingine, serikali ya Trump imekuwa ikijadili uwezekano wa kuwezesha uwekezaji wa mabilioni ya dola kutoka Magharibi katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini kama vile tantalum, bati, tungsten, dhahabu, cobalt, shaba, lithiamu na mengineyo, wakati Marekani ikiharakisha kutafuta vyanzo mbadala vya madini muhimu yanayodhibitiwa kwa kiwango kikubwa na China.

(RTRE)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *