Mchakato wa kumchagua Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa ulianza rasmi wiki iliyopita, wakati wanachama wa Umoja huo walipotakiwa kuwateua wagombea watakaochukua majukumu ya Antonio Guterres Katibu Mkuu wa sasa anayetokea Ureno.
Licha ya historia ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa kama shirika la kimataifa la amani na ushirikiano, nafasi ya Katibu Mkuu haijawahi kushikiliwa na mwanamke. Wagombea waliotangazwa hadharani kugombea nafasi hiyo ni pamoja na Grynspan, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja huo wa Biashara na Maendeleo, Rais wa zamani wa Chile Michelle Bachelet na mwanadiplomasia wa Argentina Rafael Grossi.
“Hatuhitaji kupendelewa. Kile tunachokiomba ni kutobaguliwa. Iwapo usawa utapewa kipaumbele, tutaweza kufika hapo. Hicho ndicho kitu tunachohitaji , Usawa,” alisema Grynspan, aliye na umri wa miaka 69, alipokuwa akizungumza na chombo cha habari cha Reuters mjini London. Kumekuwepo na miito ya mwanamke kuchukua nafasi hiyo na Katibu Mkuu ajae kutoka katika maeneo ya Amerika ya Kusini na maeneo ya Karibean.
Grynspan amesema Umoja wa Mataifa lazima uwe jumuishi zaidi, akiongeza kuwa wakati ilipoasisiwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ilikuwa na nchi wanachama 51, akilinganisha na wakati huu ambapo Umoja huo una nchi wanachama 193, ambako baadhi ya mataifa hayo hayakuwa na jukumu lolote wakati lilipoundwa mwaka 1945.
“Sauti hizo lazima zipate nafasi pana ya kusikika,” alisema Grynspan, akisisitiza kuwa kutoa viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja huo kwa mataifa ya Afrika na Amerika ya Kusini bila shaka ni mageuzi ambayo yakifanyika yatakaribishwa.
UN inapaswa kukubali mageuzi
Iwapo Gryspan atafanikiwa kuchukua nafasi hiyo ya kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, atabebeshwa mzigo huo wakati wa kipindi cha Donald Trump kama rais wa Marekani.
Trump ameendelea kushikilia msimamo wake kuhusu ushirikiano wa kimataifa, na ameituhumu taasisi hiyo ya dunia kushindwa kumsaidia kusuluhisha migogoro mbalimbali.
Grynspan alisisitiza kuwa ukosoaji wa Trump unaweza kuwa “wa kujenga” na si “wa kubomoa,” akisisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kujitahidi kuboresha taasisi zake akisema ni lazima ikumbatie suala la mageuzi na sio kujitetea kuhusu mageuzi hayo.