Rais Trump alitoa kauli hizo Jumanne wakati akihutubia Baraza la Mawaziri la Marekani, akirejea mashambulizi ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo nchini humo. Katika hotuba hiyo, alitishia kufunga kabisa vibali vya kuingia Marekani kwa raia kutoka mataifa kadhaa ya Afrika, akiitaja moja kwa moja Somalia kuwa miongoni mwa nchi anazozitilia shaka kiusalama.

Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre, ameonyesha kukerwa na matamshi hayo. Akizungumza katika mkutano wa kilele wa ubunifu jijini Mogadishu, Barre alisema Trump ana historia ya kutoa maneno ya kuyakera mataifa mengi, ikiwemo Nigeria na Afrika Kusini. Akaongeza kuwa si kila tamko linahitaji majibu, kwani wakati mwingine ni bora kupuuzia maneno yanayoweza kupewa uzito usiofaa.

Matamshi ya Trump yanajiri kufuatia tukio la kushambuliwa kwa walinzi wawili wa Kikosi cha National Guard jijini Washington, tukio ambalo limemfanya kuongeza vitisho dhidi ya raia wa Somalia wanaoishi Marekani

Marekani Minneapolis 2022 | Wanawake katika kitongoji cha Cedar Riverside chenye wakazi wengi wa Somalia
Wanawake wakitembea barabarani katika kitongoji chenye wasomali wengi cha Cedar-Riverside huko Minneapolis mnamo Mei 12, 2022.Picha: Jessie Wardarski/AP Photo/picture alliance

“Kauli za Trump zimetutia doa”

Kwa baadhi ya Wasomali, kauli hizo za Trump zimezua hofu, hasira na mabadiliko ya mtazamo kuhusu Marekani. Wengine wamesema maneno hayo yamewatia doa Wasomali wanaofanya kazi kwa bidii na kuchangia katika maendeleo ya Marekani, wakimtaka Trump kufikiria upya matamshi yake. Hawa ni baadhi ya wakaazi wa Mogadishu.

Miongoni mwao walisema “Mtazamo wangu kuhusu Marekani na nia ya kuishi huko umebadilika sana. Sikuwahi kufikiria kuwa rais, hasa katika muhula wake wa pili, angezungumza kwa ukali hivyo. Kwa sababu hii, sina mpango wa kwenda Marekani.”

Na huyu nae alisema “Kwa Trump, ningependa kumwambia kwamba Wasomali ni wachapakazi na watu wakujitolea, na jinsi anavyotuelezea si kweli. Sisi ni watu wema, na ninamsihi Trump afikirie upya maneno yake, kwa sababu Wasomali nchini Marekani wamechangia pakubwa katika maendeleo ya nchi.”

Somalia Mogadishu 2025 | Teksi za pikipiki na mikokoteni ya punda zikiwa kwenye barabara yenye shughuli nyingi.
Shughuli za usafirishaji kwa magari na mikokoteni inayokokotwa na punda kando ya barabara yenye shughuli nyingi huko Mogadishu, mnamo Novemba 10, 2025. Picha: Tony Karumba/AFP

“Upo ukweli” kwenye matamshi ya Trump

Hata hivyo, baadhi ya raia wameeleza kuwa ingawa matamshi ya Trump yalikuwa makali, yaligusa ukweli fulani kuhusu hali ya usalama nchini Somalia. Samira Abdullahi, mkazi wa Mogadishu ambaye ardhi yake ilitaifishwa na serikali, amesema Somalia haina utawala madhubuti na al Shabaab wanaendelea kuwatesa raia kupitia uporaji na mabomu. Hata hivyo, yoyote anayezungumza kuhusu hali hiyo, amesema, hana ruhusa kudhalilisha Wasomali.

Maafisa huko Minneapolis wamesema hawana taarifa kuhusu misako ya uhamiaji inayopangwa na serikali kuu ikiilenga jamii ya Wasomali katika eneo hilo.

Meya wa Minneapolis Jacob Frey, akijibu ripoti iliyochapishwa katika gazeti la New York Times kwamba zaidi ya maafisa 100 wa uhamiaji wa serikali kuu walikuwa tayari kuvamia jiji lake na eneo jirani la St. Paul kuwalenga wakazi wa Somalia wasio na vibali, alisema kwamba kama Misako hiyo itakuwepo au la, jamii ya Wasomali itaungwa mkono kwa kila njia inayowezekana na mamlaka za mitaa.

Kwa sasa, mjadala kuhusu matamshi na sera za Trump unaendelea kupamba moto, huku Wasomali wakieleza wasiwasi kuhusu mustakabali wao na hadhi yao kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *