
Waziri Mkuu wa Somalia, Hamza Abdi Barre, siku ya Jumatano amekosoa matamshi ya Rais wa Marekani Donald Trump yaliyolenga Somalia na wahamiaji wa Kisomali walioko Marekani.
Akizungumza katika mkutano wa ubunifu, Barre alisema Trump ametoa kauli hasi dhidi ya nchi nyingi na kwamba ni bora kutokujibu bali “kuendelea mbele.”
Trump, akizungumza katika kikao cha baraza lake la mawaziri, alidai kuwa Wasomali wamepora mabilioni ya dola ya jimbo la Minnesota bila kuchangia chochote, na akaongeza kuwa “Nchi yao haina maana, inanuka, na hatuwataki hapa.”
Kauli hizi zimeibua upinzani. Gavana wa Minnesota, Tim Walz, amewasifu Wasomali wa eneo hilo huku akimtuhumu Trump kwa “kudhalilisha kundi zima la watu waliokimbia vita na kuunda jamii yenye nguvu inayoboresha Minnesota na Marekani.”
Waziri wa mambo ya nje wa Somalia, Ali Omar, alisema Jumanne kuwa imekuwa “rahisi mno” kwa baadhi ya watu kutumia Somalia kama kisingizio cha kuficha kushindwa kwao. Alisisitiza: “Simulizi hii siyo kweli, ni dharau kwa ustahimilivu na kujitolea kwetu.” Aliwataka Wasomali “kusimama pamoja, kulinda heshima yetu, na kuonyesha ulimwengu kuwa hatutatumika kama kete ya mtu yeyote.”
Ilhan Omar, mbunge Muislamu anayewakilisha jimbo la Minnesota kwa tiketi ya chama cha Democrat amejibu mapigo kwa rais wa nchi hiyo Donald Trump baada ya kiongozi huyo kuanzisha tena mashambulizi ya matusi ya kibaguzi dhidi yake na jamii ya Wasomali wa jimbo la Minnesota.
Wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri uliofanyika jana Jumanne, Trump alianza tena kutoa kauli ya kibaguzi, akimwelezea Ilhan Omar na wahamiaji wengine Wasomali kuwa ni “takataka” tu na kuwataka waondoke Marekani.
“Tunaelekea kwenye njia isiyo sahihi kama tunaendelea kuingiza takataka nchini mwetu. Ilhan Omar ni takataka. Yeye ni takataka. Marafiki zake ni takataka,” alitamka bila ya aibu rais huyo wa Marekani.