
Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya leo mjini Tehran amechambua hotuba iliyotolewa siku chache zilizopita na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei katika hadhara ya wanawake, akielezea mtazamo wa Uislamu kuhusu wanawake, na kusisitiza kwamba Iran haijawahi kuwa na wanawake wengi wasomi na wenye maono kama ilivyo sasa, na jambo hili linaonyesha jinsi utawala wa Kiislamu hapa nchini unavyowathamini wanawake.”
Ayatullah Ahmad Khatami amesema: Katika Uislamu, wanawake wana uhuru, utambulisho na uwezekano wa kijiendeleza, lakini mtazamo wa Magharibi ni ule wa kumfanya mwanamke kuwa mfuasi na kuyeyusha utambulisho wake ndani ya wanaume. “Huko Magharibi, tunashuhudia kutoheshimiwa hadhi na utu wa mwanamke, na wanawake wamefanywa chombo na wenzo wa kushibisha tamaa za kimwili za wanaume” amesema Ayatullah Khatami.
Hatibu wa Swala ya Ijumaa ya Tehran amesisitiza kwamba: Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameviagiza vyombo vya habari kufuata mtazamo wa Uislamu na sio wa Magharibi kuhusu hadhi ya juu ya wanawake.
Katika sehemu nyingine ya hotuba zake za Swala ya Ijumaa, Ayatullah Khatami ameashiria matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi Kiislamu kuhusu propaganda za vyomboo vya habari vya Magharibi baada ya vita vya siku 12 na kumnukuu akisema: Baada ya vita hivyo, kulianzishwa propaganda kubwa za upotoshaji za adui, na Trump mwenye ndoto za mchana akishirikiana na Netanyahu mwongo walitaka kuidhihirisha Iran kama imeshindwa katika vita hivyo, lakini taifa la Iran ndilo lililoibuka na ushindi dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika vita vya siku 12.
Amewaasa Waislamu kumchamungu na kujitayarisha kwa ajili ya safari ya Akhera kwa kushikamana na ibada.
Hatibu wa Swala ya Ijuma ya Tehran amesema: “Wakati mwingine ibada ina maana maalumu, kama vile Swala, kufunga Swaumu na Hija. Kwa upande mwingine, ibada pia ina maana pana, kwa maana ya kuwa mtumishi wa Mungu katika nyanja zote za maisha, ili kila wakati Mungu anapoamuru, mtumishi wake ajisalimishe kwake kikamilifu na kutimiza ibada ya utumwa.”