Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zimeazimia kwa dhati kuchukua hatua kuelekea maendeleo na ustawi wa kikanda.
Akiashiria mazungumzo yake ya hivi majuzi na mwenzake wa Uturuki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Sayyid Abbas Araqchi amesema: Iran na Uturuki zikiwa nchi mbili muhimu za kieneo zimeazimia kuchukua hatua kuelekea amani ya kudumu, utulivu na maendeleo ya kieneo kupitia uratibu na ushirikiano wa karibu.
Akizungumzia mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan, Araghchi amisema: ” Jumapili iliyopita, nilimkaribisha Mheshimiwa Hakan Fidan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Uturuki, na ujumbe alioandamana nao mjini Tehran.”
Katika hali ya utulivu na yenye kujenga, tulipitia mwelekeo unaokua wa mahusiano baina ya nchi mbili na kusisitiza azma thabiti ya viongozi wa nchi mbili ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, biashara, nishati, usafiri, teknolojia, usalama na kiutamaduni.
Mbali na kukutana na kubadilishana mawazo na Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan alikutana pia na maafisa wengine kadhaa wa ngazi za juu akiwemo Rais Masoud Pezeshkian na Spika wa Bunge Mohamed Bagher Qalibaf. Katika ziara hiyo, pamoja na uhusiano wa pande mbili, matukio ya kikanda na masuala ya kimataifa yalijadiliwa.

Ushirikiano kati ya Iran na Uturuki katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kiusalama unaonekana kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni, na ushahidi unaonyesha kuwa mwelekeo huu unaweza kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kieneo, ingawa changamoto kama vile vikwazo na ushindani wa kijiografia bado upo.
Iran na Uturuki yakiwa madola mawili muhimu ya kikanda, katika miaka ya hivi karibuni zimejaribu kuinua uhusiano wao zaidi ya kiwango cha ushirikiano wa jadi na kuugeuza kuwa hitajio la kijiopolitiki na kisiasa.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo mbili wamesisitiza juu ya kuondolewa vikwazo vya kibiashara na kiuchumi katika vikao vya hivi karibuni, na maandalizi yanafanyika kwa ajili ya kufanyika mkutano wa tisa wa Baraza la Ushirikiano wa Juu kati ya Tehran na Ankara. Baraza hili linaweza kuwa jukwaa la uratibu mpana katika maeneo ya nishati, biashara, usafiri na teknolojia.
Kwa upande wa kiuchumi, nchi hizo mbili zimeweka lengo la kuongeza kiwango cha biashara zao hadi dola bilioni 10. Kiwango hiki sio tu lengo la kiuchumi, lakini pia ni ishara ya azma ya pamoja ya kuimarisha mahusiano wakati vikwazo na utashi wa kisiasa zimefanya ushirikiano kuwa mgumu.
Balozi wa Uturuki nchini Iran pia amesisitiza kuwa uwezo wa ushirikiano ni mkubwa na kwamba vikwazo visiwe kisingizio cha kusimamisha mchakato huu.
Katika uga wa kisiasa na kiusalama, Iran na Uturuki zimetia saini hati za maelewano za usalama zinazojumuisha ushirikiano katika kupambana na ugaidi, magendo na uhalifu wa kupangwa. Ushirikiano huu unaonyesha kuwa nchi hizi mbili zinataka kudhibiti kwa pamoja changamoto za usalama kwenye mipaka yao na katika kanda.
Nishati na usalama pia vimetajwa kuwa vichochezi vikuu vya uhusiano kati ya nchi hizi mbili, na pande zote mbili zimeelewa kuwa kuendelea kwa ushirikiano kunaweza kubadilisha mizani ya usalama na nishati katika Asia Magharibi.

Kwa mtazamo wa kikanda, Iran na Uturuki zina misimamo ya pamoja kuhusu masuala muhimu kama vile mzozo wa Syria, hali ya Gaza na matukio ya Palestina. Katika mikutano ya hivi karibuni, mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizi mbili wamesisitiza juu ya ulazima wa kusitishwa jinai dhidi ya watu wa Gaza na kuweko uratibu kwa ajili ya amani ya kudumu. Mitazamo hii ya pamoja ya kisiasa inaweza kuandaa uwanja wa mchango na nafasi ya pamoja katika kudhibiti migogoro ya kikanda.
Iran na Uturuki zina misukumo ya kuendeleza ushirikiano wao kutokana na kufanana kwao kihistoria, kiutamaduni, na kijiografia, pamoja na mahitaji yao ya pamoja katika nyanja za nishati na biashara.
Kwa ujumla, ushahidi unaonyesha kuwa hatua ya Iran na Uturuki ya kuelekea ustawi kikanda inaweza kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano. Ushirikiano huu sio tu utasaidia kuimarisha uhusiano wa pande mbili, lakini pia unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi zingine katika kanda kwa minajili ya kuleta amani ya kudumu na maendeleo ya pamoja.
Hapana shaka kuwa, iwapo nchi hizi mbili zitaweza kuondokana na changamoto zilizopo, mustakabali wa uhusiano wa Iran na Uturuki unaweza kuwa moja ya nguzo kuu za utulivu na maendeleo katika Asia Magharibi.