Sio tu kwamba deni la Kenya limekuwa gumu kulipuuza, bali pia limekuwa gumu kulifuatilia. Kwa mujibu wa IEA, jukwaa hilo limebuniwa kuonyesha kwa uwazi kiasi cha deni la Kenya, mwenendo wa ukuaji wa deni hilo, pamoja na viashiria vingine muhimu vya fedha za umma vinavyoathiri uchumi wa taifa.

Kupitia teknolojia ya wakati halisi, Kenya Debt Counter inawawezesha raia, wachambuzi wa sera, wanahabari na wadau wengine kuona mabadiliko ya deni mara yanapotokea, badala ya kutegemea takwimu zinazotolewa mara chache na serikali.

Kwame Owino, Afisa Mkuu wa Taasisi ya IEA, anasema ukizungumza kuhusu nchi tatu kubwa za Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Tanzania na Uganda; Kenya ndiyo yenye kiwango cha juu zaidi cha madeni. Iwe kwa jumla la deni lake lote au kama sehemu ya Pato la Taifa, GDP.

Tanzania na Uganda ziko chini ya Kenya

”Kama sehemu ya GDP, deni la Kenya ni takribani chini kidogo ya asilimia 70 ya Pato la Taifa. Uganda kwa mara ya mwisho nilipokagua ilikuwa karibu asilimia 55 hadi 56, na Tanzania iko chini ya asilimia 50,” alisema Owino.

Jukwaa la kidijitali la Kenya Debt Counter linatoa mgawanyo wa deni la ndani na la nje, linachambua mzigo wa ulipaji wa riba, linaonyesha uwiano wa deni kwa Pato la Taifa, na kutoa maelezo kuhusu vyanzo vikuu vya mikopo. Kwa kufanya hivyo, linaweka picha pana kuhusu hali ya uhuru wa kifedha wa nchi na nafasi ya Kenya katika masoko ya kimataifa ya fedha.

IEA inasema kuwa uzinduzi wa Kenya Debt Counter ni sehemu ya juhudi pana za kuongeza uwajibikaji wa kifedha na kuwapa wananchi taarifa sahihi wanazoweza kutumia katika kufuatilia matumizi ya serikali na kushiriki kikamilifu katika mijadala ya sera za uchumi. ”Nadhani hatupaswi kuiondoa mezani hoja ya kutafuta ufutaji wa deni,” alibainisha Owino.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanasema kwamba kutokana na uchunguzi, deni la Kenya haliripotiwi kikamilifu. Deni la Kenya limevuka shilingi trilioni 12 za Kenya, deni la nje likiwa shilingi trilioni 5.46 na deni la ndani likiwa shilingi trilioni 6.6. Wasiwasi unaongezeka kuhusu jinsi serikali inapanga kulidhibiti.

Nairobi, Kenya 2025 | Rais wa Kenya, William Ruto
Rais wa Kenya, William Ruto Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Mbunge wa Kiharu, Ndidi Nyoro, ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge yenye ushawishi ya Bajeti na Utoaji Fedha, ameonya kuhusu kile anachokiita ongezeko la deni fiche nchini Kenya.

”Katika kipindi hicho cha miaka mitatu, Kenya imekopa shilingi trilioni 3.8. Hii inamaanisha kwamba pesa ambazo Rais Mwai Kibaki alikopa katika kipindi cha miaka 10, sisi tunazikopa kila mwaka. Wale wanaoshughulikia madeni yetu, hakuna anayewakataza kukopa, lakini tafadhali tushughulikie kitabu kimoja cha madeni. Tusiiweke Kenya hatarini kwa kufungua vitabu vingine vya siri na visivyo halali vya mikopo,” alisisitiza Nyoro.

Hata hivyo, akizungumza hivi karibuni kuhusu hali ya taifa katika Bunge la Kenya, Rais Ruto alisisitiza kuwa serikali yake imeielekeza nchi kwenye uthabiti wa kiuchumi.

Umuhimu wa kupunguza matumizi

”Kenya inakabiliwa na chaguzi ngumu sana ambapo kushindwa kulipa madeni yetu kungeifanya hali mbaya iliyopo kuwa mbaya zaidi, na kukopa zaidi hakukuwa chaguo. Ilikuwa muhimu kwetu kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi, kuongeza kwa kiwango cha juu iwezekanavyo mapato ya ndani, na kudhibiti upotevu wa rasilimali,” alifafanua Ruto.

Taasisi ya IEA ina matumaini kuwa jukwaa hili litachochea mjadala mpana kuhusu kudhibiti ongezeko la deni, kuweka kipaumbele matumizi ya umma, na kuhakikisha kuwa mikopo inachangia ukuaji endelevu badala ya kuwa mzigo kwa vizazi vijavyo.

Jukwaa hilo la Kidijitali la Kenya Debt Counter linachukuliwa kuwa nyenzo muhimu ya uwazi, inayolenga kuziba pengo la taarifa na kuweka nguvu kwa umma katika kufuatilia mienendo ya kifedha ya serikali kwa njia ya wazi na inayoeleweka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *