Wanasiasa wanawake wanakabiliwa na kizingiti kikubwa cha kukosolewa na kuchukiwa na kwa kuitazama mifano tuanzie nchini Sweden nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiangaliwa kama nchi ya maendeleo, hivi sasa inatowa tahadhari.
Kwa mujibu wa gazeti la kila siku la Uingereza la The Guardian, shirika la serikali linalosimamia masuala ya usawa linasema kwamba kuna ongezeko la matukio ya chuki, vitisho na unyanyasaji dhidi ya wanasiasa wanawake kitu ambacho kinawalazimisha wengi kukaa kimya au kuchagua cha kusema au hata kujiweka pembeni na kuepuka maisha ya kuonekana mbele ya umma, kutokana na khofu.
Moja ya visa maarufu vya hivi karibuni, kinamuhusu mwanasiasa Anna-Karin Hatt nchini Sweden, mwanamama aliyejiuzulu kama kiongozi wa Center Party ambacho kinafuata siasa za wastani.
Alijiuzulu Oktoba mwaka huu baada ya kukiongoza chama hicho kwa miezi mitano tu, akiweka wazi kwamba alikuwa akipokea vitisho vingi sana na mitizamo ya kumchukia kiasi cha kutojihisi tena yuko salama, hata akiwa nyumbani kwake.
Hapa nchini Ujerumani kujiuzulu wanasiasa wanawake Tessa Ganserer ,kutoka chama cha Kijani, na naibu spika wa bunge Yvonne Magwas wa chama cha CDU kuligonga vichwa vya habari. Wote wawili walijiuzulu baada ya kuandamwa na kampeini ya kuwachafua pamoja na chuki.
Tafiti kadhaa zilizofanywa zinaonesha wanawake wanaoshikilia nyadhifa za uongozi katika mataifa mengine ya Ulaya pia wako katika nafasi ya kuandamwa zaidi na chuki.
Nchini Uholanzi kwa mfano mwanasiasa Sigrid Kaag aliyewahi kuwa waziri wa fedha na naibu waziri mkuu alijiondowa kwenye siasa baada ya kutishiwa kupigwa yeye pamoja na familia yake na sio mara moja.
Ingawa wanaume pia hukumbwa na chuki katika maisha ya umma, aina na kiwango chake vinaonekana kutofautiana. Mwaka jana, HateAid – shirika lisilo la kiserikali lenye makao yake Berlin linalotoa ushauri kwa waathiriwa wa matamshi ya chuki – kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Ufundi cha Munich kusini mwa Ujerumani, walifanya utafiti uliowahusisha watu 1,114 walioko kwenye nafasi za umma katika nyanja za siasa, elimu ya juu na vyombo vya habari.
Matokeo ya utafiti huu yaligunduwa takriban robo ya wanawake wameshapitia vitisho vya unyanyasaji wa kingono kama kubakwa tofauti na asilimia tatu ya wanaume ambao wamepitia unyanyasaji.
Katika taarifa iliyotolewa mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka huu, Umoja wa Ulaya ulisema kwamba wanawake katika mataifa ya umoja huo wanaendelea kutopewa nafasi kubwa katika ngazi za wafanya maamuzi ya kisiasa na hata katika vyama vya kisiasa.