Mkataba huo uliotiwa saini mjini Washington unalenga kuumaliza mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Hatua hiyo kulingana na Trump itazifungua hifadhi za madini muhimu ya Kongo kwa Marekani na kampuni zake.
Kabla kusainiwa kwa mkataba huo wa amani, Trump alisema ni siku nzurikwa bara la Afrika na dunia nzima kwani utawala wake umefanikiwa pale wengi waliposhindwa.
Matokeo ya mkataba huo yatakuwa ya haraka
Mkataba huo umetiwa saini huku kukiwa na taarifa kwamba mapigano bado yanaendelea mashariki mwa Kongo kati ya jeshi na wanamgambo, ila Trump alipoulizwa kuhusiana na hilo na ni lini kutakaposhuhudiwa wanamgambo na wanajeshi kujiondoa kutoka eneo hilo, alisema matokeo ya mkataba huo wa amani yatakuwa ya haraka.
“Nafikiri mutaona kwa haraka, kwa haraka sana mambo yakifanyika. Hiki ni kitu ambacho kulingana na watu wengi, kilikuwa hakiwezi kufanyika. Ila si kwamba hakiwezi kufanyika, nafikiri utakuwa muujiza mkubwa. Wanaume hawa wawili ni viongozi wakuu na wataonesha ukuu wao katika miezi na miaka kadhaa ijayo. Nafikiri mutaona matunda ya haraka, nina imani hicho ndicho kitakachofanyika,” alisema Trump.
Ukiwa umesifiwa na ikulu ya White House kama makubaliano ya kihistoria, mkataba huo kati ya Tshisekedi na Kagame uliosimamiwa na Trump, unakuja baada ya miezi kadhaa ya juhudi za kusaka amani kati ya Marekani na washirika wake, wakiwemo Umoja wa Afrika, Qatar.
Ila marais hao wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, hawakutazamana wala kupeana mikono wakati wa hafla hiyo ya kutia saini mkataba huo, iliyodumu kwa karibu dakika hamsini hivi.
Kagame na Tshisekedi lakini walitoa matamko ya kutia moyo huku Kagame akimsifu Trump kwa kuchukua hatua hiyo ya kuleta amani huku Tshisekedi akisema anatumai kuwa kutiwa saini kwa mkataba huo hakutokuwa njia ambayo amani itakuwa ndoto, bali njia ya kupatikana kwa amani ya kweli.
Lakini mkataba huo uliosimamiwa na Trump hauko salama na huenda ukafeli kufikisha mwisho mapigano kwani Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, imezongwa na mapigano ya kwa miongo kadhaa, kukiwa na zaidi ya makundi 100 ya wanamgambo, kubwa na lenye uwezo miongoni mwao likiwa lile la waasi wa M23.
Mashariki ya Kongo yamezewa mate
Trump alikutana na Tshisekedi na Kagame kwa mikutano tofauti na kila mmoja kabla kufanya mkutano mwengine wakiwa wote watatu uliofuatiwa na kutiwa saini kwa mkataba huo wa usitishaji huo wa mapigano.
Trump amekuwa akilimezea mate mno eneo la mashariki mwa Kongo lililo na utajiri wa madini muhimu, wakati ambapo Washington inatafuta njia za kuizidi maarifa China ili ipate madini nadra yanayotumika katika utengenezaji wa ndege za kivita, simu na vifaa vyengine muhimu.
China inashikilia asilimia 70 ya uchimbaji wa madini muhimu duniani na inadhibiti asilimia 90 ya utengenezaji wa bidhaa kutokana na madini hayo.
Mwaka huu mapigano hayo yalizidi huku waasi wa M23 wakiiteka miji muhimu ya eneo la mashariki mwa Kongo ya Goma na Bukavu. Hatua hiyo ya M23 iliipelekea hali ya kibinadamu huko mashariki kuwa mbaya zaidi huku mamilioni wakiachwa bila makao.
Vyanzo: APE/Reuters