Waziri mkuu wa India Narendra Modi na rais Vladmir Putin wa Urusi,wamefanya mazungumzo leo Ijumaa wakati ukifanyika mkutano wa kilele wa kila mwaka kati ya mataifa hayo mawili, ukilenga kuimarisha mahusiano.
Mwanzoni mwa mazungumzo ya viongozi hao wa wawili rais Putin amemfahamisha waziri mkuu Narendra Modi kuhusu operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine pamoja na juhudi za amani zinazoongozwa na Marekani kumaliza vita hivyo.
India na Urusi zashadidia mahusiano yao
Kwenye mkutano wa kilele wa 23 wa kuimarisha mahusiano kati ya mataifa hayo mawili,ambao umekuja katika kipindi muhimu, Marekani ikionekana kushinikiza juu ya kupatikana amani huku ikitafuta ushirikiano wa kimataifa, rais Vladmir Putin amemshukuru waziri mkuu Modi kwa kuonesha mshikamano na Urusi.
“Tumepata fursa na umenipa nafasi ya kuzungumza kwa kina zaidi kuhusu kile kinachoendelea katika vita ya Ukraine na kuhusu hatua tunazozichukuwa kwa pamoja na washirika wengine ikiwemo Marekani kuelekea uwezekekano wa kupata mwafaka wa amani kwenye mgogoro huu”
Kiongozi huyo wa Urusi aliendelea kupongeza mahusiano ya nchi yake na India huku New Delhi ikiielezea Moscow kama mshirika muhimu wa kimkakati.
Waziri mkuu Narendra Modi ameitaja ziara ya Putin kuwa kubwa yenye kubeba umuhimu wa kihistoria kwa kuzingatia kwamba ni miaka 25 tangu Putin alipoitembelea India mwaka 2001.
Rais wa Urusi na Waziri Mkuu wa India kukutana New Delhi kwa mazungumzo
Modi amesema ziara hiyo iliweka msingi wa mahusiano hayo ya ushirika wa kimkakati kati ya Mataifa hayo huku pia akiweka wazi kwamba India ni mshirika wa kutegemewa katika kuleta amani.
“India sio nchi isiyotegemea upande wowote,India ni nchi inayoegemea upande wa amani. Tunaunga mkono juhudi zote za amani tunasimama bega kwa bega linapohusika suala la amani”
Mikataba kadhaa yasainiwa New Delhi
India na Urusi zimesaini makubaliano kadhaa ya ushirikiano katika sekta mbali mbali ikiwemo za kibiashara na kijeshi huku rais Vladmir Putin akisisitiza kwamba Moscow itaendelea kuiuzia mafuta New Delhi bila kutatizwa.
Ushirikiano huu wa India na Urusi unaonesha ni kwa jinsi gani sasa NewDelhi italazimika kuweka urari katika mahusiano yake baina ya Moscow na Marekani hasa kwa kuzingatia kwamba Marekani nimekuwa ikiishinikiza India kuutathmini upya uhusiano wake na Moscow.