Anaandika Askofu Bagonza

TUMEISHAANDAMANA; GEN-Z TUPE NAFASI TUJUTE KWANZA.

Leo tarehe 6 Desemba, ni siku yangu ya kuzaliwa. Sina furaha kama ninavyokuwaga na furaha katika siku hii. Hii ni kwa sababu moyo wangu unawaza maandamano yenye utashi lakini yasiyo na kibali. Nawasihi Gen-Z watafakari haya:

1. Balozi zote na mataifa mbalimbali duniani tayari yameandamana hata kabla ya tarehe 9 kwa kulaani kilichotokea Tanzania.

2. Mashirika ya ndege ya kimataifa yameandamana kwa kusitisha kutua DSM, KIA na Zanzibar na yanarudishia abiria nauli zao.

3. Polisi, wakuu wa mikoa na wilaya wanaandamana bila utaratibu. Huyu anafunika, yule anafunua. Huyu anafoka, yule anapotezea.

4. Watekaji wanaandamana, wanateka mapadre, watawa, mabalozi wa amani na mazingira hata watoto wa chekechea. Ni kama Wanawalazimisha maaskofu waingie barabarani kuandamana. Tutaicheka Kongo tena Subutu!

5. Wana DSM wameandamana tayari. Kila mtu anakunbuka kwenda nyumbani kula Krismas. Hata Wazaramo wanakubali kwao ni Maneromango. Hata mlinda mlango kaondoka.

6. Mashehe wameandamana kupinga maandamano. Wanatema cheche utafikiri rais ni wa kwao tu. Wanamtetea rais kuliko wanavyoitetea serikali. Rais bila serikali ni sawa na Shehe bila Msikiti. Tuheshimiane: RAIS NI WETU SOTE, MSIMTEKE.

7. Niwakumbushe kama mmesahau. Malalamiko yoooote yaliyopo si mapya. Yamekuwapo miaka yote na maandamano hayakutokea. Kipya ni kimoja tu: UTEKAJI. Mpaka sasa aliyeulaani ni CHALAMILA. Amesaliti?
Tambueni kwa hakika; asiyekemea utekaji ndiye mtekaji.

8. Tanzania tumeijenga kwa miaka 60, tukaibomoa kwa siku tatu. Hatujaridhika kuwa tumebomoa sawasawa. Dola haitaki kukubali na Gen Z hawataki. Serikali ni yetu na Gen Z ni wetu. Tumeishaandamana. Sasa tuzungumze.
Tuwajibishane. Vyeo vyetu viwe vidogo kuliko taifa letu.

9. Ukisingiziwa uzinzi usijitetee. Ni heshima kuliko kusingiziwa uanithi.
Hatujasingiziwa kuiba binadamu. Tumeambiwa tumeiba kura na tumeua watu. Siri tunayo moyoni. Tumejitetea vya kutosha. Kila tukisukuma mzigo mita mbili mbele; tunarudishwa nyuma mita tano. Nashauri sasa tuwe wapole na tusimwage damu tena. Risasi inaua mtu; haiui mawazo yake.

10. “Kabla ya wale waliomkimbiza mama mkwe wako hawajarudi, usitambe kuwa mama mkwe wako huwa ana mbio kweli kweli”. Hakuna aliyejua tutafika hapa. Kuna msomaji wangu kaniita mimi kuwa ni FARA kwa kuwa ninayaandika. Nimemjibu kuwa nakaribia kuwa FARANGA. Faranga zote duniani zinaizidi shilingi yetu isipokuwa ya Burundi. Tusipokubali ukweli, hata Burundi watatuhifadhi na faranga yao.

11. Serikali isitishe utekaji na kufoka. Gen-Z wasitishe maandamano. Wafiwa wakabidhiwe miili, majivu, udongo au maji ili tarehe 9 badala ya maandamano iwe siku ya mazishi kitaifa. Serikali isijishauri bali ipate mtu aishauri. Isipokubali kushindwa, ITASHINDWA.
Wajaluo wanasisitiza, “kusimanisha saa hakuzuii jua kuendelea na safari”.

HAPPY BIRTHDAY TO ME.
Hongera Ma Dorothea kwa kuzaa Fara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *