
Hayo ni kwa zingatio la mazungumzo kati ya Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Waziri Mkuu wa Ubelgiji Bart De Wever na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen mjini Brussels siku ya Ijumaa. Merz kwa mara nyingine alimuhakikishia De Wever kwamba hatari zinazotokana na kuruhusu mali zilizodhibitwa chini ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya, ambazo nyingi zinashikiliwa na Ubelgiji, zitagawanywa kwa usawa kati ya nchi wanachama. Ili kuanzisha mkopo kwa ajili ya Ukraine, taasisi za kifedha kote Umoja wa Ulaya zitalazimika kuhamisha mali zote za serikali ya Urusi zilizoshikiliwa zenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 245 kwenye mfuko maalumu wa utoaji na uratibu wa mkopo. Ukraine itapokea takribani Euro bilioni 90 kwa awamu ili kugharamia mahitaji ya kifedha na ya kijeshi katika miaka ya 2026 na 2027.