Turki Al-Faisal, mwanamfalme wa Saudi Arabia ambaye pia ni mkuu wa zamani wa shirika la kijasusi la Saudia amesisitiza katika mkutano wa kimataifa huko Abu Dhabi kwamba, kinyume na wanavyodai baadhi ya watu, tishio hasa la eneo hili la Asia Magharibi si Iran bali ni utawala wa Kizayuni ambao ndio unaohatarisha utulivu wa eneo hili lote.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Turki Al-Faisal amebainisha hayo kwenye hotuba yake aliyoitoa katika mkutano wa “Mashariki ya Kati na Afrika” ulioitishwa na Taasisi ya Milken na kusema: “Maoni yangu mimi ni kwamba, bila ya shaka ni Israel ndiyo inayosababisha matatizo na lazima idhibitiwe na Marekani.”

Al-Faisal amegusia uvamizi wa mara kwa mara unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon, Ghaza na pia Syria, akisema kwamba, vitendo hivyo vinaonesha kwamba utawala wa Kizayuni “unahisi una nguvu sana na haushibitiki.”

Mkuu huyo wa zamani wa Shirika la Ujasusi la Saudia ameendelea kusema: “Israel inaishambulia Syria karibu kila siku, inaendelea na mashambulizi yake dhidi ya Wapalestina huko Ghaza au Ukingo wa Magharibi na hata inafanya mashambulizi nchini Lebanon, licha ya kuweko makubaliano ya kusitisha vita, yote haya ni ushahidi usiopingika kwamba Israel ndiyo inayotishia usalama wa eneo hili na si Iran kama wanavyodai baadhi ya watu.”

Turki al-Faisal amezungumzia pia mashambulizi ya Israel dhidi ya ujumbe wa Hamas huko Qatar katika miezi ya hivi karibuni akisema kwamba shambulio hilo kwa kweli lilikuwa “onyo zito” kwa kila mtu kwamba nchi za Ghuba ya Uajemi lazima zichukue hatua za pamoja za kulinda usalama wao na kwamba “ushirikiano kwenye masuala ya ulinzi katika Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (GCC) si kitu jipya.”

Matamshi yake hayo yalikuwa ni kuashiria taarifa ya nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi kwamba zimo katika kuandaa mpango wa kuunda mfumo wa pamoja wa ulinzi wa anga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *