
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi nane za Kiislamu wameeleza wasi wasi wao mkubwa kutokana na matamshi ya hivi karibuni ya maafisa wa Israel kuhusiana na kufunguliwa kwa upande mmoja kivuko cha Rafah na kuwahamishia wakaazi wa Gaza nchini Misri.
Mawaziri hao wamepinga vikali jaribio lolote la kuwaondoa kwa nguvu watu wa Palestina katika ardhi yao.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Misri, Jordan, Imarati, Indonesia, Pakistan, Uturuki na Qatar wametangaza katika taarifa yao ya pamoja kwamba, mpango wa utawala wa Israel wa kufungua kwa upande mmoja kivuko cha Rafah kwa lengo la kuwatimulia wakazi wa Gaza nchini Misri ni hatua ya kutia wasiwasi na isiyokubalika.
Mawaziri hao wamesisitiza kuwa, jaribio lolote la kutaka kuwaondoa kwa nguvu wananchi wa Palestina katika ardhi yao ni jambo lisilokubalika na ni lazima kuwekwe mazingira ili waendelee kubaki katika ardhi yao na kushiriki katika ujenzi na maendeleo ya nchi yao.
Aidha wametaka kutekelezwa kikamilifu mpango wa amani wa Rais Donald Trump wa Marekani, ambao unasisitiza kufunguliwa kwa njia mbili za kivuko cha Rafah, uhuru wa kutembea kwa watu, na sio kuwalazimisha kuondoka majumbani mwao.
Pia wametaka kuheshimiwa kikamilifu kwa usitishaji mapigano, kukomesha mateso ya raia, kuwezesha kuingia kwa misaada ya kibinadamu huko Gaza, kuanza kwa mchakato wa ujenzi mpya, na kuandaliwa mazingira ya kukabidhiwa majukumu kwa Mamlaka ya Palestina.