Rais Vladimir Putin wa Russia amefanya ziara nchini India kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya nchi mbili.

Rais wa Russia aliwasili New Delhi Alhamisi iliyopita, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini India tangu kuanza kwa vita vya Ukraine mwaka 2022. Ziara hiyo ya siku mbili imefanyika lengo likiwa ni kuimarisha uhusiano wa kiulinzi na kibiashara kati ya nchi mbili. Katika ziara yake hiyo nchini India, Putin alifuatana na ujumbe wa ngazi za juu, akiwemo Waziri wake wa Ulinzi. Marais wa India na Russia pia wameshiriki katika vikao rasmi na vya kiuchumi, ukiwemo mkutano wa 23 wa kila mwaka kati ya nchi hizo mbili.

Pande mbili zimesaini hati 10 za mapatano na mikataba zaidi ya 15 ya kibiashara, itakayofafanua mwelekeo wa kimkakati wa ushirikiano wa kiuchumi hadi mwaka 2030, ambapo kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kinaweza kufikia dola bilioni 100. Moja ya maeneo makuu ya majadiliano ya pande mbili ni ushirikiano katika uga wa ulinzi. Uhusiano wa nishati na biashara pia ni sehemu muhimu ya safari  ya Rais wa Russia nchini India. 

Rais Putin akiwa na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa india Narendra Modi (Kulia)

Wakati huo huo, Rais wa Russia ameitembelea New Delhi katika hali ambayo India inakabiliwa na mashinikizo makubwa ya serikali ya Trump kwa sababu ya hatua yake ya kununua mafuta ya Russia ya bei nafuu. India imekuwa miongoni mwa wateja wakubwa wa mafuta ya Russia tangu mwaka 2022, na hivyo imeweza kuokoa mabilioni ya dola kwa kununua mafuta ya bei nafuu. Pamoja na hayo, India imepunguza kuagiza mafuta kutoka Russia kutokana na vikwazo vya Marekani kwa makampuni makubwa ya Russia kama vile Rosneft na Lukoil. Serikali ya Trump mwezi Agosti mwaka huu ilitoza ushuru wa asilimia 50 kwa bidhaa nyingi za India na kutaja sababu ya kufanya hivyo kuwa ni utegemezi wa India kwa mafuta ya Russia na kusaidia kifedha katika  vita vya Ukraine. Hatua hiyo imeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa viongozi wa India, kwa sababu mkataba wowote mpya wa nishati au ulinzi utakaotiwa saini kati ya nchi hiyo na Russia unaweza kufuatiwa na majibu makali wa Washington.

Licha ya mashinikizo hayo, Russia imetangaza kuwa haihofii hatua za Marekani na imejikita katika kupanua uhusiano na India. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa uhusiano wa kistratejia wa nchi mbili hizo hauwezi kusitishwa hata kama biashara ya mafuta itapungua; kwa sababu Russia inaendelea kudhamini vipuri kwa kajili ya zana kongwe za kijeshi za India. Wakati huo huo, kiwango cha biashara kati ya nchi mbili kilifikia dola bilioni 68.7 mwaka 2024-2025 yaani karibu mara sita ya kiwango cha kabla ya janga la maambukizi ya Corona. Hata hivyo, mauzo ya India kwa Russia ni chini ya dola bilioni 5 kwa mwaka, na New Delhi inataka kuwa na sehemu kubwa katika soko la dawa, magari na huduma nyinginezo huko Russia. 

Mbali na masuala ya kiuchumi na ulinzi, safari ya sasa ya Putin nchini India pia ina umuhimu wa kijiografia na kisiasa. Kwa India, kukutana na Putin ni ishara ya kujitawala kimkakati na kudumisha mlingano katika mahusiano ya kimataifa. Kwa Putin, ambaye husafiri nje ya nchi kwa nadra, safari ya India inatuma ujumbe wa wazi kuhusu umuhimu wa mahusiano na New Delhi. Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya India ameelezea uhusiano wa nchi hiyo na Russia kuwa ndio “imara zaidi katika zama za sasa” na kusisitiza kwamba ziara hiyo inapaswa kuonekana katika muktadha wa uhusiano wa pande mbili.

Bila shaka, ziara ya Vladimir Putin nchini India haiwezi kuonekana kama kupuuza vitisho vya utawala wa Trump kwa New Delhi tu, lakini pia imefanyika ndani ya mfumo wa sera ya kimkakati ya India ya kulinda kujitawala kwake na mlingano katika mahusiano ya kimataifa. Katika miaka ya hivi karibuni, India imejaribu kupanga uhusiano wake na mataifa makubwa kwa njia ambayo sio tu kwamba inalinda maslahi yake ya kiuchumi na usalama, lakini pia inaepuka kuwa tegemezi kupita kiasi kwa upande mmoja.

Vitisho vya Trump, hasa kuweka ushuru mkubwa kwa bidhaa za India na mashinikizo dhidi ya New Delhi kwa ajili ya kupunguza ununuzi wa mafuta ya Russia, ni ukweli ambao India haiwezi kuupuuza. Hatua hizi zinaonyesha kwamba, Washington haifurahishwi na uhusiano wa nishati na ulinzi baina ya India na Russia na inauona kama aina ya msaada usio wa moja kwa moja kwa Russia katika vita nchini Ukraine. Hata hivyo, India iko katika hali ambayo haiiruhusu kujitenga kabisa na Russia. Sababu ya kwanza ni mahitaji ya haraka ya silaha na vipuri vya Russia, ambavyo havina mbadala wa haraka na wa bei rahisi katika soko la kimataifa. Sababu ya pili ni mabilioni yaliyookolewa na India katika miaka ya hivi karibuni kwa kununua mafuta ya bei rahisi kutoka Russia, ambayo yamesaidia sana uchumi wa nchi hiyo.

Putin akiwa na safarini nchini India

Kwa ujumla, ziara ya Putin nchini India inaonyesha juhudi za nchi hizo mbili za kutaka kulinda na kuimarisha uhusiano wa kimkakati licha ya mashinikizo makubwa ya kimataifa. Ushirikiano katika sekta za ulinzi, biashara ya nishati na masuala ya kijiografia na kisiasa unabaki kuwa lengo kuu la mahusiano hayo, na nchi zote mbili zinahitajiana katika ngazi ya kimkakati, licha ya mashinikizo ya Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *