Marekani na Rwanda zimetiliana saini mkataba wa miaka mitano wa thamani ya dola milioni 228 kwa ajili ya sekta ya afya katika taifa hilo la Afrika Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema, makubaliano haya ni ya pili kutiwa saini chini ya utawala wa Rais Donald Trump yanayohusu mbinu mpya ya misaada ya nje ya nchi (“America First Global Health Strategy”.)

Kenya ni nchi ya kwanza kutiliana saini na Marekani makubaliano hayo yaliyozinduliwa mwezi Septemba ambapo  utawala wa Trump unataka kuboresha hali katika sekta za afya na kujitegemea zenyewe katika kusimamia sekta hiyo kwenye  nchi hizo lengwa. Fedha hizo, dola milioni 228 zitatolewa na serikali zote mbili za Rwanda na Marekani.

USA Washington D.C. | Rais Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Ron Sachs/Newscom World/IMAGO

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema, mkataba wa Rwanda unalenga jitihada na maono ya kina ya kuokoa maisha, kuimarisha mfumo wa afya wa Rwanda.

Mkataba wa ufadhili wa afya ulitiwa saini siku moja baada ya Rais wa Rwanda Paul Kagame na mwenzake wa Jamhuri yake ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi kutia saini makubaliano ya amani yaliyosimamiwa na Marekani juu ya kuumaliza mzozo wa mashariki mwa Kongo.

Chini ya mpango huo mpya wa afya, Marekani itatoa hadi dola milioni 158 kwa Rwanda kwa ajili ya kupambana na VVU/UKIMWI, magonjwa mengine ya kuambukiza na Malaria. Marekani imesema fedha hizo pia zitasaida kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kukabiliana na magonjwa ya milipuko.

Kwa upande wake, serikali ya Rwanda imesema, inapanga kuongeza uwekezaji wake wa ndani katika sekta yake ya afya kwa dola milioni 70, ikichukua uwajibikaji zaidi wa kifedha wakati ambapo Marekani ikiendelea kupunguza usaidizi wake hatua kwa hatua.

Mkataba mpya wa Afya Duniani

Marekani imesema, mkataba huo unahusisha kushirikiana na Rwanda katika kuanzisha mfumo wa kutumia droni aina ya Zipline kwa ajili ya kufikisha bidhaa za matibabu ya kuokoa maisha pale zinapohitajika.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Oliver Nduhungirehe amesema, “Mkataba huo unasisitiza azma ya Rwanda ya kujenga mfumo wa afya unaojitegemea, unaobadilika, na unaowezeshwa na teknolojia.”

Kwa upande wa Kenya, Marekani itatoa zaidi ya dola bilioni 1.6 kwenye mfumo wa afya wa Kenya chini ya mkataba huo mpya wa miaka mitano uliotiwa saini mjini Washington.

Utawala wa Rais Donald Trump mnamo mwezi Septemba ulitangaza mkakati mpya wa “Afya Duniani” katika sera yake ya Marekani Kwanza, ambao unatoa wito kwa mataifa maskini kutwaa majukumu makubwa katika kupambana na VVU/UKIMWI, Malaria, Kifua kikuu na Polio na kuweza kujitegemea zenyewe na hatimaye kubadili kabisa mazoea ya kupokea misaada kutoka nje.

USA Washington D.C. 2025 | William Ruto , viongozi wengine wa Afrika na Rais Trump
Kushoto: Rais wa Kenya William Ruto. Kulia: Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Chip Somodevilla/Getty Images/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na Rais wa Kenya William Ruto walitia saini makubaliano hayo mjini Washington ambapo Ruto aliahidi kuongeza matumizi ya ndani ya nchi yake kwenye sekta ya afya hadi dola milioni 850 katika kipindi cha miaka mitano.

Nchi nyingine za Afrika zinatarajiwa kutia saini mikataba kama hiyo katika siku zijazo, maafisa wa Marekani wamesema.

Mfumo mpya wa Marekani wa “Afya Duniani” umeanzishwa baada ya kuvunjwa kwa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani USAID mapema mwaka huu wa 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *