Kundi la wanajeshi wa Benin leo Jumapili limetangaza kupitia kituo cha utangazaji cha serikali kwamba limefanya mapinduzi na kumuengua madrakani Rais Patrice Talon, na kumteua Luteni Kanali Pascal Tigri kuongoza kamati mpya ya kijeshi.

Ubalozi wa Ufaransa nchini Benin pia umeeleza katika taarifa yake kwamba milio ya risasi imesikika katika kambi ya Camp Guezo, karibu na makazi ya rais.

Ubalozi huo umewataka raia wa Ufaransa kusalia majumbani hadi itakapotolewa taarifa nyingine kuhusu hali ya mambo. 

Talon, mfanyabiashara wa zamani, amehudumu kama Rais wa Benin tangu mwaka 2016 na alichaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili wa urais mwaka 2021.

Adama Gaye, Mkurugenzi wa zamani wa Mawasiliano katika Jumuiya ya ECOWAS ameiambia televisheni ya al Jazeera yenye makao mjini Doha, Qatar kwamba mapinduzi ya leo si jambo la kushangaza kwa yoyote na kwamba Benin ilikuwa katika mvutano mkubwa wa kisiasa huku viongozi wengi wa upinzani wakifungwa jela.

Ameongeza kuwa, Rais aliyepinduliwa Patric Talon alifanikiwa “kuwaondoa watu muhimu katika chama cha upinzani, ikiwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Benin, Thomas Boni Yayi” na tayari alikuwa amemteua waziri wake wa sasa wa fedha kuchukua hatamu baada ya uchaguzi ujao. 

Kundi la wanajeshi lililotangaza kumpindua Rais wa Benin limesema kuwa mipaka yote nchini humo imefungwa na vyama vya kisiasa vimesimamishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *