Umoja wa Afrika, AU umelaani vikali mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyofanywa na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF yaliyoua makumi ya watu wakiwemo watoto katika mji wa Kalogi kusini mwa Sudan.

Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, Mkuu wa Kamisheni ya Afrika, Mahmoud Youssouf, amesema, “amechukizwa na uhalifu unaorudiwa na unaozidi kutendeka dhidi ya raia katika mkoa huo.”

Tamko hilo limeeleza kwamba, mkuu huyo wa Kamisheni ya AU “analaani kwa lugha kali zaidi mashambulizi hayo ya kutisha yaliyoripotiwa” katika mji wa Kalogi, ambayo yanadaiwa kuwaua “zaidi ya raia 100, wakiwemo makumi ya wanawake na watoto katika kituo cha chekechea.”

Tamko hilo limeongeza kuwa, Youssouf “ana wasiwasi mkubwa” kuhusu ripoti za kuendelea kudondoshwa mabomu, mashambulizi ya droni, na mashambulio dhidi ya miundombinu muhimu ya kiraia, zikiwemo hospitali na skuli.

Mkuu huyo wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika vilevile ametaka kusitishwa mapigano mara moja, na kuhimiza upatikanaji wa misaada ya kibinadamu “bila vikwazo.”

Kwa mujibu wa Esamuddin al-Sayed, mkuu wa kitengo cha utawala katika mji wa Kalogi, mashambulizi hayo ambayo yalifanywa na RSF siku ya Alkhamisi katika mji huo unaodhibitiwa na jeshi, yalihusisha hujuma tatu; “ya kwanza ililenga chekechea, kisha hospitali na mara ya tatu wakati watu walipojaribu kuwaokoa watoto”. 

Al-Sayed ameyahusisha mashambulio hayo na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) na mshirika wake, tawi la Harakati ya Kaskazini ya Ukombozi ya Watu wa Sudan (SPLM-N) linaloongozwa na Abdelaziz al Hilu, ambalo linadhibiti sehemu kubwa ya Kordofan Kusini na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Blue Nile…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *