
RB Leipzig waliibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Eintracht Frankfurt, lakini gumzo kubwa lilikuwa jina moja: Yan Diomande.
Kijana huyo raia wa Ivory Coast alifunga hattrick, akituma ujumbe wa wazi kuelekea mechi za hatua ya makundi ya Kombe la Dunia FIFA 2026 kati ya Ivory Coast na Ujerumani.
Kwa kufunga mabao matatu akiwa na umri wa miaka 19 na siku 22, Diomande ameweka rekodi ya kuwa mfungaji wa hattrick mwenye umri mdogo wa pili katika historia ya Ligi Kuu ya Ujerumani Bundesliga. Ni hatua inayomweka rasmi kwenye ramani ya vipaji vinavyoinuka barani Ulaya.
Mashabiki na wachambuzi wa soka wanamtaja kama “lulu mpya wa Leipzig” wakiona mustakabali wake ukiwa na mwanga mkubwa.
Kasi yake, uwezo wa kupiga vyenga na kumalizia mashambulizi kwa ustadi vinamfanya kuwa tishio kwa mabeki wa Bundesliga na mwiba mkali kwa wapinzani wa Ivory Coast katika michuano ya Kombe la Dunia.
Tayari vilabu vikubwa barani Ulaya ikiwemo Liverpool, Tottenham Hotspur na FC Barcelona vimeanza kumrushia ndoano, wakiona nafasi ya kumvuta kijana huyo kabla jina lake halijawa kubwa zaidi.
Kwa hattrick yake dhidi ya “Eagles” Diomande ametuma onyo kwa Julian Nagelsmann na kikosi chake cha Ujerumani. Ikiwa ataendelea kuonyesha fomu nzuri, mechi ya Ivory Coast dhidi ya Ujerumani inaweza kuwa moja ya michezo ya kusisimua zaidi katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Timu ya taifa ya Ujerumani imepangwa kundi E pamoja na Ivory Coast, Ecuador na Curaçao katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia FIFA 2026.