JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MAWASILIANO YA RAISI, IKULU
Dodoma
08 Desemba, 2025
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
(KWA KUTOLEWA MARA MOJA)
TANZANIA NA MAREKANI ZASONGA MBELE KUKAMILISHA MAKUBALIANO MAKUBWA YA UWEKEZAJI
Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, leo amefanya mazungumzo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz, Ikulu ya Chamwino, kwa lengo la kusukuma mbele maeneo muhimu ya ushirikiano wa pande mbili na kuimarisha dhamira ya pamoja ya ushirikiano wa kisasa wenye manufaa kwa pande zote.
Balozi Lentz, akiwa ameambatana na Afisa Mshauri wa Siasa na Uchumi, amesisitiza dhamira ya Marekani kuimarisha upya uhusiano wao na kuongezea nguvu ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, na kiusalama kati ya mataifa hayo mawili.
> “Marekani imejikita kwenye ushirikiano usiotegemea misaada, bali unaojengwa juu ya maendeleo ya pamoja,” alisema Balozi Lentz.
Mazungumzo yalijikita katika miradi mikubwa yenye uhusiano na wawekezaji wa Marekani, ambayo imekuwa ikijadiliwa.
Pande zote zilikiri kuwa majadiliano ya hatua za mwisho za uwekezaji wa miradi mikuu—mradi wa LNG na mradi wa madini ya Nickel—yanaingia hatua ya mwisho kabla ya kutiwa saini. Mradi wa tatu uliojadiliwa ulikuwa wa madini ya Graphite Mahenge, ambao bado unaendelea kushughulikiwa.
Rais aliipongeza Marekani kwa dhamira yake na akaihahakikishia ujumbe wa Marekani kwamba Tanzania imejipanga kukamilisha hatua zilizobaki katika mchakato huo.
“Kama nchi isiyofungamana na upande wowote, Tanzania iko wazi, tayari na imejitoa kushirikiana na washirika wote wanaoheshimu uhuru wetu na kushirikiana katika dira yetu ya maendeleo,” alisema Rais Samia.
“Miradi hii mikakati ni ya umuhimu wa kitaifa, na tumejidhatiti kuikamilisha ili iweze kufungua ajira, uwekezaji, na ustawi endelevu kwa wananchi wetu.”
Rais pia alibainisha kuwa zaidi ya kampuni 400 za Marekani zinafanya shughuli nchini Tanzania—ikiwa ni ishara ya uimara wa nchi, mazingira bora ya uwekezaji na uhusiano wa muda mrefu wa kiuchumi kati ya Tanzania na Marekani.
Mbali na uwekezaji, kikao hicho pia kiligusia masuala mapana zaidi ya ushirikiano, ikiwemo:
Utulivu wa kisiasa
Usalama wa kikanda
Mageuzi ya kiuchumi
Ukuaji wa sekta binafsi
Ushirikiano katika sekta ya afya
Mabadilishano kati ya watu kwa watu
Balozi Lentz alimpongeza Rais Samia kwa dira na mipango madhubuti kupitia Dira ya Maendeleo 2050, akisisitiza kwamba Serikali ya Marekani iko tayari kuunga mkono utekelezaji wake na kuimarisha falsafa ya 4R inayoongoza sera za Rais katika utawala.
Pande zote mbili zilikubaliana kuwa mawasiliano thabiti, ushirikiano wa karibu na hatua za haraka katika makubaliano ya uwekezaji ni muhimu kufungua fursa zaidi katika uhusiano wa Tanzania na Marekani.
Mkutano huu ni hatua muhimu katika kubadili na kuimarisha uhusiano wa kiuwekezaji kati ya Tanzania na Marekani.
Dhamira hiyo iliyothibitishwa na pande zote inaashiria mwanzo wa ushirikiano wa kisasa unaojengwa juu ya:ustawi wa pamoja,kuheshimiana,uwazi, naushirika wa sekta binafsi.
Miradi Mikuu ya Uwekezaji
1. Mradi wa LNG – Thamani ya Makadirio: Dola bilioni 42
Mradi wa gesi asilia unaohusisha makampuni ya kimataifa; umelenga kufungua rasilimali kubwa za gesi katika pwani ya Tanzania. Ukikamilika, utaleta mapato makubwa ya serikali, ajira kwa maelfu ya watu na kuiweka Tanzania katika nafasi ya juu duniani kama muuzaji mkubwa wa LNG.
2. Mradi wa Madini ya Nickel – Thamani: Dola milioni 942
Uwekezaji katika madini muhimu unaopatikana Ngara, ukijikita kwenye Nickel—madini muhimu kwa betri za magari ya umeme. Mradi utachochea:
uongezaji wa thamani,
viwanda,usambazaji wa nishati safi duniani,
mapato ya mauzo nje ya nchi.
3. Mradi wa Graphite Mahenge – Thamani: Dola milioni 300
Moja ya miradi mikubwa duniani ya Graphite ya daraja la juu kwa ajili ya viwanda vya betri na nishati mbadala. Mradi utaimarisha nafasi ya Tanzania kama mtoa mkubwa wa Graphite yenye ubora kwa uzalishaji wa betri.
Imetiwa saini na:
Shaaban Kissu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Cc:-Manara Tv
imetafsiriwa na Eddy Rashid