Katika kipindi cha mwaka 2025, takriban wanafunzi 700 ambao ni sehemu ya jumla ya wanafunzi 1,400 kutoka familia zisizojiweza kiuchumi, wamefuzu somo la lugha ya Kijerumani katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya jimbo la Homabay, ikiwa ni katika harakati za kuitambua zaidi lugha ya kigeni ya Kijerumani.
Kwa mujibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, kupitia Katibu Mkuu wake, Dokta Raymond Omollo, mpango huu ulio chini ya makubaliano ya mwaka 2024 kati ya Kenya na Ujerumani unalenga ajira miongoni mwa vijana. Omollo anasema waliofuzu wanalenga kuendeleza masomo na nafasi za ajira ughaibuni, lengo likiwa ni kujikwamua kimaisha.
”Mwaka jana, Kenya na Ujerumani walitia saini makubaliano ya ajira na kuna hitaji kubwa la Wakenya kujiunga na soko la ajira la Ujerumani. Mojawapo ya hitaji ni kujifunza Kijerumani na utamaduni wao. Wanafunzi wanaosoma Kijerumani wanahitajika kupitia kozi na kufuzu,” alifafanua Dokta Omollo.
Awamu ya kwanza ilikuwa na wanafunzi 710
Kupitia mpango wa kitaifa wa kuwawezesha wajane, makundi ya vijana wa kike na kiume yalitambuliwa na kujiunga na mpango huu. Awamu ya kwanza ya wanafunzi 710 walioanza masomo ya Kijerumani mwezi Septemba mwaka 2024 walifanya mtihani wao mnamo mwezi Julai mwaka 2025 na kufuzu mnamo mwezi Septemba.
Inagharimu takriban shilingi 140,000 za Kenya kusomea kozi ya Kijerumani kwa kipindi cha miezi sita na hivyo mpango huu wa serikali ni habari njema kwa wanafunzi wengi. Kadhalika, taasisi iliyoidhinishwa kuwapa mitihani wanafunzi hao na kuwapa vyeti vya kufuzu ni inLEGAS yenye makao makuu nchini Ujerumani. Taasisi hii ilianza kufanya kazi nchini Kenya kuanzia mwezi Aprili mwaka 2024.
Akizungumza na DW, mmoja wa wanafunzi anayesoma lugha ya kijerumani anasema baada ya kumaliza masomo wanaenda nje ya nchi, kwani huko kila mtu anatamani kufika, na kwamba kupitia programu hiyo, binafsi anaona kuna nuru mbele yake.
“Kuja kwangu hapa ilikuwa niongeze juhudi nipate ujuzi unaohitajika ambao ni kujifunza Kijerumani ili niweze kufanya kazi nje, na niweze kuisaidia familia yangu,” alisema mwanafunzi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
Mbali na somo la Kijerumani, wanafunzi husika pia wanapewa mafunzo maalum kuhusu matumizi ya fedha na ujuzi mbalimbali ili kuwaandaa wanapopata nafasi ughaibuni, hali inayolenga kuwaunganisha vijana kutoka Kenya na soko la ajira kimataifa nchini Ujerumani na mataifa ya bara la Ulaya yanayozungumza lugha hii.
Miongoni mwa sekta zainazolengwa katika maandalizi ya ajira ni afya, benki, Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari, nishati, uhandisi, ufundi wa mabomba na sekta ya magari. Kulingana na Dokta Omollo, Bodi ya Ujerumani inayoandaa mitihani ya Kijerumani imesisitiza kuwa, ni sharti kwa mtahiniwa kufaulu na kupata cheti chenye kiwango cha B1 katika lugha ya Kijerumani ili aweze kunufaika na nafasi hizi.
Vigezo muhimu kuzingatiwa
“Kupitia makubaliano haya ya Ujerumani, nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya, imewafungulia milango kwa sababu Ujerumani huhitaji wafanyakazi wa kigeni zaidi ya 400,000 kila mwaka kujaza uhaba wa wafanyakazi ambao umechangiwa na idadi ya watu wanaozeeka,” alisisitiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani.
Miongoni mwa vigezo vya kuwachagua wanafunzi waliojiunga na mpango huu wa masomo ya Kijerumani kando na kutokea katika kundi la wajane, mwanafunzi alihitajika kuwa na cheti cha kidato cha nne na kuwa chini ya umri wa miaka 35, kwa soko la ajira Ujerumani linahitaji nguvu kazi ya vijana.
Akizungumza na kundi la wanafunzi wa Chuo cha Tom Mboya mnamo mwezi Septemba mwaka 2025, Dokta Omollo aliwahimiza kuendelea kuongeza juhudi za kutimiza ndoto zao za maishani na kuvunja minyororo inayowafifisha moyo kutokana na chimbuko lao, na waendelee kuweka juhudi za mafanikio ya siku za usoni.
“Kama taifa, tumechukua hatua madhubuti na nyinyi ni sehemu ya kundi la waanzilishi ambao wataenda kunufaika nje ya ukurasa huu mpya. Makubaliano haya yanatoa fursa na kulegeza taratibu za uhamiaji kwa kuhakikisha visa za muda mrefu, za makaazi ya muda hadi fursa za kuongeza masomo, unalindwa dhidi ya mawakala walaghai, ili safari yako iwe salama, iliyopangwa na ya heshima,” alibainisha Dokta Omollo.
Mbali na mpango huo wa chuoni, vile vile wimbi la kujifunza lugha ya Kijerumani pia limeanza kushika kasi Kisumu, kwani ziara ya Meya wa mji wa Gertshofen nchini Ujerumani, Michael Worle mapema mwezi Novemba, 2025, ulifungua ukurasa mpya kwa wenyeji kujifunza lugha hiyo.
Serikali ya Jimbo la Kisumu kwa ushirikiano na Meya Worle, wamezindua kitengo cha mafunzo ya Kijerumani maarufu kama German Language Corner katika Maktaba Kuu ya jimbo hilo, hatua inayolenga kukuza lugha hiyo miongoni mwa wakaazi hasa vijana. Nancy Ochieng, Mratibu wa Maktaba hiyo anasema wamefurahishwa na hatua hiyo muhimu, kwani utaleta mafanikio makubwa.
“Naamini huu ni mwanzo mpya unaotazamiwa kuleta mafanikio tele katika siku za usoni. Ni wazi kwamba Kisumu imefunguka katika jukwaa la kimataifa na tunavyojulikana kuwa watu tunaopenda kusoma na idadi kubwa ya wasomi nina hamu sana kuona matokeo ya hatua hii,” alisema Ochieng.
Fursa katika soko la ajira
Profesa Charles Omondi, Naibu Kansela wa Chuo Kikuu cha Tom Mboya, anasisitiza pakubwa kuhusu mfumo huu wa uimarishaji akisema ni fursa nzuri kwa wanafunzi kutambua sio tu kwa misingi ya ujuzi na utaalamu, bali kupitia kuelewa lugha ya soko la ajira wanalolilenga.
Anabainisha kuwa hatua hii inatoa fursa pana kwa wanaosaka nafasi za ajira kuwa na kitu tofauti kinachowaweka katika nafasi bora zaidi ya soko la ajira hasa ughabuni.
“Endapo huzungumzi lugha husika, hatua ya kwanza ya mawasiliano huwezi hata kupata kazi. Hata kama una ujuzi wa ufundi wa mabomba, hata kama unajua ufundi wa umeme, uhandishi au wapimaji wa ardhi,” alifafanua Profesa Charles Omondi.
Wengi wa wanafunzi walionufaika na mpango wa mafunzo ya Kijerumani katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya Homabay, wanatoka katika familia zinazoongozwa na wajane, chini ya mpango maalum wa msaada kwa kundi hili la wanajamii kote nchini Kenya.