Kanda inayonyesha wanajeshi waliojihami kwa bunduki wakitumia fimbo kuwacharaza wafuasi wa mgombea urais Robert Kyagulanyi anayefahamika zaidi kwa jina Bobi Wine, ambao nusra wamgeukie yeye mwenyewe imeibua hisia mseto za hofu, hasira na wasiwasi kuhusu hali ya wapinzani nchini Uganda.
Wengi wanaelezea kuwa msimu huu wa uchaguzi umefikia kiwango cha juu cha ghasia na machafuko za uchaguzi ambazo ikiwa hazitadhibitiwa,huenda vifo na majeraha zaidi vikashuhudiwa. Mmoja kati ya walinzi wa Bobi Wine kwa jina Daniel Oyorwoth almaarufu Dan Magic ameonekana akivuja damu kwenye paji lake la uso akiwa ameshikiliwa na mgombea huyo.
Kisa kilichotokea mjini Gulu Kaskazini mwa Uganda alikokuwa ameenda kufanya kampeni mgombea huyo kwa mujibu wa ratiba rasmi ya tume ya uchaguzi. Akiwahutubia wandishi habari kabla ya kuanza kampeni zake jijiji Kampala hii leo, mgombea huyo ameleezea vitendo hivyo kuwa vya kikatili na ni vitisho vya utawala ambao unategemea zaidi majeshi kubakia madarakani badala ya kukubali ushidani wa kidemokrasia.
Anakosoa jamii ya kimataifa kwa kutoshtumu utawala wa rais Museveni kwa vitendo hivyo ambavyo anataja kuwa kinyume sheria za kimataifa za kulinda haki za binadamu.
Polisi wasitumiwe dola kuwatendea hujuma waganda
Mgombea mwengine wa urais kwa tiketi ya chama cha ANT Jenerali Mugisha Muntu amewashauri wanajeshi na askari polisi wasikubali kutumiwa na dola kuwatendea hujuma raia wa kawaida.
Huku tume ya haki za binadamu ya Uganda ikihimiza vyombo vya usalama kutotumia nguvu za kupindukia dhidi ya watu wanaoshiriki kampeni zinazoendelea,raia mbalimbali wanakosoa uhusika wa moja kwa moja wa wanajeshi katika masuala ya siasa. Mwenyekiti wa tume hiyo Mariam Nagadya naye amekiri kwamba hata maisha yake mwenyewe yamo hatarini kwa kukosoa maovu yanayofanywa na vyombo vya usalama na hata raia ambao wamedhihirisha ghadhabu zao kuhusu kuzorota kwa haki za binadamu nchini.
Kwa upande wake rais Yoweri Museveni ambaye anatetea kiti hicho amendelea kuwambia wapigaji kura kwenye mikutano yake ya kampeni kwamba hawezi kuacha mazingira ya amani ambayo amejitolea mhanga miaka yote kuyajenga yaharibiwe na watu ambao hawajatoa mchango wowote kuhakikisha hiyo amani.
Lakini kwa wapinzani wake, matamshi hayo wanayatafsiri kuwa ni vitisho kwa raia. Wanadai , Museveni hutegemea zaidi kujenga hofu miongoni mwa raia anaposema kuwa bila yeye kubaki kwenye utawala, Uganda haiwezi kuwa na amani na badala yake itatumbukia katika msukosuko wa kisiasa ambao utasababisha machafuko.
Kinachozidi kuwaghdhabisha raia wa Uganda ni kukaa kimya kwa tume ya uchaguzi ambayo haijatoa tamko lolote kuhusu kisa hicho cha wanajeshi kumshambulia Bobi Wine na walinzi wake kwa fimbo.
