Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amewataka wananchi waendelee kuliamini na kuliacha Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi wa kutokewa kwa aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.

Chalamila amesema hayo Ijumaa, Desemba 5, 2025 wakati akijibu swali aliloulizwa kwenye mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari ambao ni wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Swali hilo limetaka kujua kama Chalamila amewahi kwenda kumtembelea mama yake Polepole na au Polepole mwenyewe yupo wapi kwani alitoweka akiwa mkoani mwake. Oktoba 6, 2025, taarifa zilisambaa mitandaoni zikidai Polepole aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo (CCM) ametekwa na watu wasiojulikana akiwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam na mpaka sasa hakuna taarifa zozote juu yake.

Akijibu swali hilo, Chalamila amesema matatizo katika mkoa huo yapo mengi na hawezi kwenda kumtembelea kila mmoja na huo hautakuwa uongozi.

“Polepole alikuwa Balozi, mimi kama mkuu wa mkoa sijui alijiuzulu akiwa nchi gani,” amesema na akisisitiza hakuna utaratibu wa Balozi anapokuja nchini kwenda kuripoti kwa mkuu wa mkoa. Amesema alisikia tu kwamba amechukuliwa:”Kumbe alikuwa Dar es Salaam…Sina taarifa zozote ninazoweza kumzungumzia (Polepole) zaidi nilikuwa naangalia YouTube tu yale anayoyasema kwani hayakuonyesha alikuwa anazungumzia akiwa wapi.

Chalamila amesema majibu yaliyotolewa na Polisi:”Tuwape muda waendelee na uchunguzi, kama nilivyosema upelelezi unategemea na aina ya tukio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *