Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar amesema mawasiliano baina ya Doha na harakati ya Hamas yalianza miaka 10 hadi 13 iliyopita kwa lengo la kurahisisha juhudi za kusitisha mapigano na kupeleka misaada ya kibinadamu Ghaza.

Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al-Thani ameeleza hayo katika mkutano wa Doha kuongeza kuwa mawasiliano hayo yamekuwa ya uwazi na yamefanyika chini ya usimamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel; na missada ambayo imekuwa ikitolewa na Qatar haikuwa kwa ajili ya Hamas bali kwa watu wa Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar ameendelea kueleza kwamba, baadhi ya wanasiasa wamejaribu kutumia uhusiano huo ili kujipatia manufaa ya muda mfupi na kusambaza taarifa za kupotosha kuhusu Qatar, kwa hivyo shutuma zozote kwamba Qatar inaifadhili kifedha Hamas hazina msingi.

Amesisitiza kwamba nafasi na mchango wa Qatar umesimama juu ya msingi wa kupunguza mivutano na kufikia amani katika eneo, kwa sababu inaamini kwamba kuwa na maingiliano na pande zote, za kiserikali na zisizo za kiserikali, ni muhimu ili kufikia suluhu ya kudumu.

Al-Thani amebainisha kuwa shambulio lililofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Doha lilikuja wakati Qatar ilikuwa ikijaribu kuwashawishi Hamas wakubali pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump.

Amesema Qatar haitafadhili kifedha ujenzi upya wa kile ambacho wengine wamekiharibu, lakini haitawaacha kamwe watu wa Palestina bila kuwapatia msaada…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *