
Nyota wa Liverpool Mohamed Salah yupo katika hali ya sintofahamu kuhusu mustakabali wake ndani ya majogoo wa Liverpool, baada ya kuonyesha wazi kutoridhishwa na kuachwa benchi katika sare ya 3-3 dhidi ya Leeds United.
Salah hakuchezeshwa kabisa katika mechi hiyo, ikiwa ni mara ya tatu mfululizo ameanza benchi.
Baada ya mechi kukamilika, alitoa kauli akisema klabu “imemtupa chini ya basi” na kudai hana tena uhusiano mzuri na kocha Arne Slot.
Kauli zake zimeibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na wachambuzi, huku wengine wakihisi anakaribia kuondoka Anfield.
Wayne Rooney amemshutumu Salah kwa “kuharibu taswira yake” na kudai maneno yake yalikuwa ya kudhalilisha klabu na wachezaji wenzake.
Salah mwenye umri wa miaka 33 sasa, anatarajiwa kujiunga na timu ya taifa ya Misri kwa michuano ya AFCON 2025, jambo linaloongeza mashaka kama ataichezea tena Liverpool kabla ya mashindano hayo kuanza.
Klabu za Saudi Arabia zinaripotiwa kufuatilia kwa karibu hali hii, zikitarajia kumshawishi iwapo ataamua kuondoka.