Mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, unatarajiwa kuangazia jinsi ya kujibu mapendekezo ya Marekani ya kumaliza vita na Urusi.
Ukraine na washirika wake wa Ulaya pia huenda wakasisitiza kwamba makubaliano yoyote ya usitishaji mapigano yanapaswa kuja na dhamana za usalama kutoka Marekani na ”muungano wa walio tayari” ulioitishwa na Uingereza na Ufaransa, huku pia ukipinga kuachilia baadhi ya maeneo kuwa chini ya udhibiti wa Urusi.
Mara kwa mara, Starmer amesema Ukraine lazima iruhusiwe kuamua mustakabali wake, huku mmoja wa mawaziri wake wakuu akisema jana Jumapili kwamba nchi hiyo inapaswa kuchukuwa hatua katika uvamizi huo wa Urusi.
Ziara hiyo ya Zelensky inakuja baada ya maafisa wake kuhitimisha siku tatu za mazungumzo na wenzao wa Marekani juu ya mapendekezo hayo huku Ikulu ya White House ikiishinikiza Ukraine kukubali makubaliano hayo.
Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa Telegram, Umerov aliyeongoza ujumbe huo wa Ukraine katika mazungumzo na maafisa hao wa Marekani, amesema jukumu kuu la timu yao katika mazungumzo hayo ya hivi karibuni lilikuwa kupokea taarifa kamili kuhusu mazungumo kati ya Marekani na Urusi na rasimu zote za mapendekezo ya sasa.
Umerov pia amesema pamoja na washirika wao, lazima wafanye kila linalowezekana
kukomesha vita hivyo kwa heshima.
Hapo jana katika hotuba yake ya kila jioni, Rais Volodymyr Zelenskyalisema kuwa
Umerov, na mkuu wa wafanyakazi wake Andrii Hnatov, walikuwa wanarejea kumuarifu yaliojiri.
”Natarajia taarifa za kina kutoka kwao juu ya kila kitu ambacho kilisemwa kwa wajumbe wa Marekani huko Moscow, na kuhusu mitazamo ambayo Wamarekani wako tayari kurekebisha katika mazungumzo na sisi na Warusi.”
Viongozi saba wa EU wataka kuharakishwa kutumia mali ya Urusi kwa Ukraine
Viongozi kutoka mataifa saba wanachama wa Umoja wa Ulaya leo wameuhimiza Umoja huo kuchukuwa hatua za haraka kuhusu pendekezo la kutumia mali ya Urusi iliyofungiwa kuifadhili Ukraine.
Katika barua iliyotumwa kwa Rais wa Baraza Kuu la Umoja huo Antonio Costa na mwenzake wa Halmashauri kuu ya Umoja huo Ursula von der Leyen, viongozi hao kutoka Estonia, Finland, Ireland, Latvia, Lithuania, Poland na Sweden wamesema kuiunga mkono Ukraine katika mapambano yao ya uhuru sio tu wajibu wa kimaadili lakini pia kwa ajili ya maslahi yao binafsi.