Syria yapambana kupona baada ya miongo ya utawala wa AssadSyria yapambana kupona baada ya miongo ya utawala wa Assad

Mwaka mmoja uliopita, Mohammad Marwan alijikuta akitembea kwa kuyumba, bila viatu na akiwa amechanganyikiwa, akitoka katika gereza hatari la Saydnaya karibu na Damascus wakati waasi walipoliteka na kuwaachia wafungwa.

Alikamatwa mwaka 2018 kwa kukwepa utumishi wa lazima ya jeshini, na baada ya kupitia magereza mengine manne, Saydnaya ndiyo iliyoacha alama ya kudumu katika mwili na akili yake.

Marwan anakumbuka maafisa gerezani wakipokea wafungwa wapya kwa vipigo na mshtuko wa umeme, wakiwaambia hawakustahili haki yoyote. Aliporejea nyumbani Desemba 8, 2024, familia na marafiki walimlaki kwa furaha kuu.

Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye bado anapambana kupona mateso yake: kifua kuuma, kushindwa kupumua vizuri—baadaye ikagundulika ni kifua kikuu—na msongo wa mawazo uliomnyima usingizi.

Sasa anapata tiba ya kifua kikuu na msaada wa kisaikolojia katika kituo cha Homs kinachowahudumia wafungwa wa zamani.

Nchi inayojaribu kupona

Syria yenyewe pia inahangaika kujiponya baada ya utawala wa familia ya Assad uliodumu miaka 50 kuanguka, ukiacha maiti zaidi ya nusu milioni, mamilioni wakikimbia makazi yao na nchi ikiwa imegawanyika.

Kuanguka kwa Assad kulikuja kwa mshangao hata kwa waasi waliomwangusha. Novemba 2024, makundi ya kaskazini-magharibi, yakiongozwa na Hayat Tahrir al-Sham (HTS) na kiongozi wake wa zamani Ahmad al-Sharaa—sasa rais wa mpito—yalianzisha mashambulizi mkoani Aleppo.

Syria, Damascus 2025 | Gwaride la kijeshi kwa kumbukumbu ya mwaka wa kwanza wa kuanguka kwa Bashar al-Assad.
Mwonekano wa juu wa droni unaonyesha wanajeshi wakifanya maonyesho wakati wa gwaride la kijeshi, huku Wasyria wakiadhimisha mwaka wa kwanza tangu kuanguka kwa Bashar al-Assad, mjini Damascus, Syria, Desemba 8, 2025.Picha: Khalil Ashawi/REUTERS

Walistaajabu kuona jeshi la Syria likisambaratika haraka, kuanzia Aleppo hadi Hama na Homs, likiacha wazi njia ya kuelekea Damascus.

Wakati huo, makundi ya kusini nayo yalielekea mji mkuu. Waasi waliuteka mji wa Damascus Desemba 8 huku Assad akikimbizwa na wanajeshi wa Urusi kuelekea Moscow. Ingawa Urusi haikumuokoa kijeshi, imebaki na ushawishi mkubwa nchini kupitia vituo vyake vya kijeshi.

Mafanikio ya diplomasia, changamoto za ndani

Tangu kuchukua uongozi kwa ghafla, al-Sharaa amefungua njia mpya za kidiplomasia, akijenga mahusiano na mataifa ya Magharibi na Kiarabu yaliyomkataa Assad. Novemba mwaka huu, alikua rais wa kwanza wa Syria kutembelea Washington tangu mwaka 1946.

Hata hivyo, mafanikio haya yamegubikwa na vurugu za kimadhehebu ambazo zimeua mamia ya raia wa jamii za Alawite na Druze. Katika mkoa wa Sweida, Wadruze wameanzisha utawala na jeshi lao la kujitegemea.

Mvutano unaendelea kati ya serikali mpya na vikosi vinavyoongozwa na Wakurdi kaskazini-mashariki, licha ya makubaliano ya Machi ya kuunganisha majeshi.

Israel, ingawa imeambiwa haitafutwi vita, bado ina wasiwasi na serikali mpya ya Kiislamu. Imechukua eneo lililokuwa likisimamiwa na Umoja wa Mataifa kusini, na mashambulizi yake ya anga bado yanaendelea.

Uchumi dhaifu na ndoto za ujenzi upya

Uchumi wa Syria bado umedorora licha ya vikwazo vingi vya Magharibi kuondolewa. Nchi za Ghuba zimeahidi kuwekeza katika ujenzi mpya lakini miradi mikubwa bado haijaonekana. Benki ya Dunia inakadiria kuwa ujenzi wa maeneo yaliyoharibiwa na vita utagharimu dola bilioni 216.

Assad akimbia nchi, waasi waukamata Damascus

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kwa sasa, ujenzi upya umeachwa mikononi mwa watu binafsi—wamiliki wa nyumba na biashara wanaojaribu kurekebisha makazi yao kwa kipato chao wenyewe.

Katika kambi ya Yarmouk karibu na Damascus, iliyoharibiwa vibaya na vita, wakazi wa zamani wameanza kurudi taratibu. Kwenye barabara kuu pekee, baadhi ya majengo yameanza kurejeshwa na maduka kufunguliwa, lakini maeneo mengi bado ni magofu.

Tumaini jipya, hofu ile ile

Maher al-Homsi, anayerekebisha nyumba yake, analalamika kuwa mwaka mzima umepita bila hatua za kweli za serikali kuondoa magofu na kujenga upya.

Jirani yake, Etab al-Hawari, anaona bado ni mapema kuilaumu serikali mpya, akisema waliikuta nchi ikiwa tupu—mabenki yakiwa yameporwa na miundombinu kuharibiwa.

Bassam Dimashqi, daktari wa meno, anasema hali ni bora zaidi sasa kwa sababu angalau kuna aina fulani ya uhuru, lakini bado ana wasiwasi juu ya usalama na uchumi. Anasisitiza kuwa ustawi wa kiuchumi utaanza tu pale serikali itakaporejesha usalama wa kudumu ili kuvutia wawekezaji.

Kwa Marwan, maisha baada ya Assad ni “bora zaidi,” lakini bado anakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi. Kazi anazopata hulipa wastani wa pauni 50,000–60,000 za Syria kwa siku—sawa na takriban dola 5.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *