Wakati wa uzinduzi wa Mtazamo wa Hali ya Kibinadamu Duniani kwa mwaka 2026, mratibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na misaada ya kibinadamu Tom Fletcher, alisema bado kuna maumivu katika kila upande na akaonya kuwa watu robo bilioni wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu wakati ufadhili ukiwa umepungua hadi kiwango cha chini zaidi katika muda wa muongo mmoja.
Akizungumza katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Fletcher amesema ombi la mwaka jana lilifanikiwa tu kupata msaada wa dola bilioni 12 na kuifanya ripoti hiyo kuwa ya huzuni kuchapisha.
“Mnamo mwaka 2025, njaa iliongezeka. Bajeti ya chakula ilipunguzwa licha ya nja kuzikumba sehemu za Sudan na Gaza. Mifumo ya afya ilisambaratika. Maelfu walipoteza huduma muhimu. Milipuko ya magonjwa iliongezeka. Mamilioni ya watu walikosa chakula muhimu, huduma za afya na ulinzi. Mipango ya kulinda wanawake na wasichana ilipunguzwa. Mamia ya mashirika ya misaada yalifungwa, na zaidi ya wafanyikazi 380 wa msaada waliuawa, hii ikiwa idadi ya juu zaidi kurekodiwa.”
Fletcher alionya kuwa mfumo wa kibinadamu unadhoofika na kwamba juhudi ya msaada zimezidiwa, zinapata ufadhili mdogo na kushambuliwa. Pia amesema ni asilimia 20 tu ya wito wao ulioungwa mkono.
UN yataka kuchangisha dola bilioni 33 kusaidia watu milioni 135, 2026
Licha ya hilo, Fletcher amesema mashirika ya misaada yalifikia watu milioni 98 mwaka jana na kuongeza kuwa anajipa moyo kutokana na imani ambayo viongozi wengi wanayo, akiwemo rais wa Marekani, kwamba mwaka 2026 utakuwa mwaka wa kuleta amani, ambao unaweza kuleta fursa ya kipekee ya kufanya jambo lisilo la kawaida.
Lengo la Umoja wa Mataifa kwa 2026 ni kuokoa maisha ya watu milioni 87 kupitia mipango 29 katika nchi 50. Mahitaji yanajumuisha dola bilioni 4 kwa watu milioni tatu katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu, dola bilioni 2.8 kwa watu milioni 20 nchini Sudan, dola bilioni 2 kwa Wasudan milioni saba waliokimbia makazi yao kuvuka mipaka, na dola bilioni 1.4 kufikia watu milioni 4.9 walioathiriwa na mgogoro wa Myanmar.
Hatimaye Umoja wa Mataifa ungependa kuchangisha dola bilioni 33 kusaidia watu milioni 135 mwaka 2026 lakini unafahamu kwamba lengo lake la jumla linaweza kuwa gumu kufikiwa, kutokana na hatua ya Rais wa Marekani Donald Trump kukatiza misaada ya kigeni.
Fletcher amesema wito uliopewa kipaombele zaidi umejikita katika maamuzi ya kufa na kupona na kuongeza kuwa anatumai Marekani itaona maamuzi na mageuzi yaliofanywa ili kuboresha ufanisi wa misaada, na kuchagua kujitolea tena kutoa misaada.
