
Kiongozi huyo aidha ametaka Israel kusitisha mashambulizi na kuruhusu misaada zaidi kuingia Gaza. Haya yanajiri wakati serikali ya Israel ikisema iko tayari kuingia awamu mpya ya makubaliano hayo, huku ikiitaka Hamas kurudisha mabaki ya mateka wa mwisho wa Israel.
Husam Badran wa kitengo cha kisiasa cha Hamas ameitaka Israel kutekeleza “masharti yote ya awamu ya kwanza,” ikiwemo kusitisha ubomoaji wa nyumba za Wapalestina katika maeneo yanayodhibitiwa na Israel.
Tangu kusitishwa kwa mapigano tarehe 10 Oktoba, maafisa wa afya wa Palestina wanasema Wapalestina wasiopungua 376 wameuawa katika operesheni za kijeshi za Israel.
Israel nayo imeilaumu Hamas kwa kukiuka makubaliano ya usitishaji vita, ikisema mashambulizi yake ni kujibu mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake au watu wanaokaribia sana eneo lililowekwa katika makubaliano, ingawa waliouawa ni pamoja na wanawake na watoto, na baadhi ya mashambulizi yametokea hata kwenye “maeneo salama.”
Kauli ya Hamas inatolewa wakati mpango unaoongozwa na Marekani kuhusu mustakabali wa Gaza ukizidi kupata kasi katika wiki za hivi karibuni.