Wahusika wakuu – ambao ni Israel, wanamgambo wa Hamas, Marekani na wapatanishi wa kimataifa ikiwemo Qatar, wanaingia katika awamu ya pili ya mazungumzo ya kufikia makubaliano mapya yatakayotoa mwelekeo mpya katika Mashariki ya Kati.
Mpango wa rais Donald Trump wa nukta 20, ulioidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, unaeleza nia ya kuondoa utawala wa Hamas Gaza. Iwapo utafanikiwa, dunia itashuhudia Gaza mpya isiyokuwa na silaha wala wanamgambo, itakayosimamiwa na vikosi vya kimataifa, mahusiano bora zaidi kati ya Israel na mataifa ya Kiarabu, na huenda pia ukafungua njia ya uhuru wa Palestina.
Lakini ukifeli, Gaza huenda ikaendelea kubaki njia panda kwa miaka mingi ijayo huku Hamas ikiendelea kuidhibiti.
Netanyahu kujadili na Trump hatma ya mpango wa amani ya Gaza
Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, Waziri Mkuu wa Qatar na mpatanishi muhimu, amesema mazungumzo yako katika kipindi kigumu. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kusafiri kuelekea Washington Desemba 29 kukutana na rais Trump kujadili hatua zinazofuata.
Duru zinaeleza kuwa Trump anapanga kutoa awamu ya pili ya mpango huo kabla ya Krismasi, huku kukiwa na mashaka kuhusu uwezekano wa hilo kutimia.
Rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sissi huenda pia akaungana na viongozi wenzake kujadili hatma ya Ukanda huo. Katika ziara ya Netanyahu ya siku nane Washington, atakutana na Makamu wa Rais JD Vance, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth.
RSF: Israel ni muuaji mkubwa wa waandishi habari duniani
Wakati huo huo, wanajeshi wa Israel wamewaua kwa kuwapiga risasi Wapalestina wawili waliodaiwa kuwarushia mawe katika eneo linalokaliwa kimabavu la Ukingo wa Magharibi.
Tukio hili linajiri wakati Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA), Philippe Lazzarini, akikosoa hatua ya Israel kuzuilia mali za shirika hilo Mashariki mwa Jerusalem. Polisi waliiambia AFP kwamba hatua hiyo ni sehemu ya operesheni ya kukusanya madeni.
Kwengineko, shirika la kimataifa la Waandishi Wasio na Mipaka (RSF) limesema Israel imehusika na karibu nusu ya mauaji ya waandishi wa habari mwaka huu, huku 29 wakidaiwa kuuawa na jeshi lake. Katika ripoti yake ya kila mwaka, RSF yenye makao yake Paris limesema jumla ya waandishi 67 waliuawa duniani, ikilinganishwa na 66 mwaka uliopita.
Jeshi la Israel linachangia asilimia 43 ya mauaji hayo, na kulifanya kuwa adui nambari moja kwa waandishi wa habari. Shambulizi baya zaidi lililotekelezwa na Israel lilitokea katika hospitali moja Kusini mwa Gaza Agosti 25, na kuua waandishi watano.
Kwa ujumla, tangu vita kati ya Israel na Hamas kuanza Oktoba 7, 2023, takriban waandishi 220 wameuawa, na hii imeifanya Israel kuwa kile ambacho RSF inataja kuwa muuaji mkubwa wa waandishi wa habari kwa miaka mitatu mfululizo.
