Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, amesema Jumanne (09.12.2025) kuwa mkakati mpya wa usalama wa utawala wa Rais Donald Trump unaonyesha wazi haja ya Ulaya kuwa huru zaidi na Marekani katika masuala ya usalama. Merz amesisitiza kuwa wazo kwamba demokrasia ya Ulaya inahitaji kuokolewa halina msingi.
Alisema baadhi ya vipengele vya nyaraka hiyo vinaeleweka, lakini “kuna sehemu ambazo kwa mtazamo wa Ulaya hazikubaliki kabisa.”
Merz aliwaambia waandishi wa habari katika jiji la Mainz kwamba haoni sababu yoyote kwa Marekani kudai kutaka kuokoa demokrasia ya Ulaya.
“Baadhi yake yanaeleweka, baadhi yake yanafahamika. Baadhi yake hayakubaliki kwetu kutoka mtazamo wa Kiulaya. Sioni haja ya Wamarekani sasa kutaka kuokoa demokrasia barani Ulaya. Kama ingewezekana kuokolewa, tungelisimamia sisi wenyewe”, alisema Merz.
Mkakati huo wa usalama wa Marekani, uliotolewa Ijumaa, unaichora Ulaya kama mshirika mnyonge, na unatoa ishara za kuunga mkono vyama vya siasa za mrengo mkali wa kulia. Pia unakosoa vikali sera za Ulaya kuhusu uhuru wa kujieleza na uhamiaji.
Je, Ulaya inaelekea pabaya?
Friedrich Merz, ambaye anaongoza taifa lenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Ulaya na lenye uchumi mkubwa zaidi katika Umoja wa Ulaya, alisema hakushangazwa na maudhui ya mkakati huo, kwani yanafuata msimamo ulioonekana katika hotuba ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, aliyotoa Munich mwezi Februari.
Jumatatu, Rais wa Baraza la Ulaya, António Costa, alionya Marekani kuacha kuingilia mambo ya ndani ya Ulaya, akisema kwamba ni raia wa Ulaya pekee wanaoweza kuamua vyama vitakavyowatawala.
Rais wa Marekani Donald Trump kwa mara nyingine tena alikosoa vikali Ulaya siku ya Jumatatu, akisema inaelekea “katika mwelekeo mbaya.” Akiongeza kuwa Marekani haikutaka Ulaya “kubadilika sana,” bila kueleza hasa alichomaanisha.
Chini ya shinikizo la Rais Trump, nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO, ikiwemo Ujerumani, zilifikia makubaliano mwezi Juni kuongeza kwa kiwango kikubwa malengo ya matumizi ya ulinzi ya muungano huo.