Hali hiyo ni siku chache tu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kukutana na viongozi wa Rwanda na Congo kutangaza amani.

Katika taarifa ya Jumatatu jioni, Umoja wa Mataifa ulisema kiasi ya watu 74 wameuawa, wengi wao wakiwa raia, na wengine 83 kulazwa hospitalini kutokana na mapigano yaliyokithiri. Maafisa wa eneo hilo wanasema waasi wa M23 wamekuwa wakipambana na jeshi la Congo na makundi ya kujitolea ya Wazalendo katika vijiji vya kaskazini mwa Uvira, baada ya kuteka mji wa Luvungi ambao ulikuwa mstari wa mbele tangu Februari. Mapigano makali pia yameripotiwa karibu na Sange na Kiliba.

Rwanda imeendelea kukanusha kuunga mkono waasi, lakini Marekani na Umoja wa Mataifa wanasema ushahidi wa uungwaji mkono huo uko wazi. Hata kabla ya machafuko mapya, mzozo huo ulikuwa tayari umewahamisha watu zaidi ya milioni 1.2.

Mwaliko wa Marais Paul Kagame na Félix Tshisekedi mjini Washington

Wiki iliyopita, Trump aliwaalika Marais Paul Kagame na Félix Tshisekedimjini Washington kwa hafla ya kutia saini makubaliano ya amani yaliyofadhiliwa na Marekani na Qatar, akidai serikali yake “imefanikiwa pale wengine waliposhindwa.”

USA Washington D.C. 2025 | Trump empfängt Kagame und Tshisekedi zur Friedensabkommen-Unterzeichnung
Trump awapokea Kagame na Tshisekedi kwa ajili ya kusaini makubaliano ya amaniPicha: Chip Somodevilla/Getty Images/AFP

Lakini katika hotuba yake kwa wabunge jana Jumatatu, Rais Félix Tshisekedi aliishutumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano hayo,”Siku moja tu baada ya kusaini makubaliano, vikosi vya Ulinzi vya Rwanda vilifanya mashambulizi makubwa ya silaha kutoka mji wa Bugarama, vikisababisha madhara makubwa ya kibinadamu na mali hasa katika maeneo ya Kaziba, Katogota na Lubarika na hivyo kukikuka usitishaji wa mapigano.”

Wakazi walisema mapigano yalizidi kushika kasi huko Kivu Kusini wiki iliyopita licha ya makubaliano ya amani. Jeshi la Congo na waasi wa M23 wameendelea kushutumiana kukiuka masharti ya usitishaji mapigano yaliyokubaliwa mapema mwaka huu.

Umoja wa Mataifa, unasema waasi wa M23 wanasaidiwa na karibu wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda

Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, waasi wa M23 wanasaidiwa na karibu wanajeshi 4,000 kutoka Rwanda, na mara kadhaa wametishia kuendelea na mashambulizi hadi Kinshasa, mji mkuu wa Congo ulioko umbali wa takribani kilomita 1,600 mashariki.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema Jumatatu kuwa ina wasiwasi mkubwa kuhusu machafuko yanayoendelea, ikisisitiza kuwa Rwanda “lazima izuie ongezeko la mapigano.”

Afisa mwandamizi wa utawala wa Trump alisema Marekani inafuatilia kwa karibu na kufanya kazi na pande zote mbili, akiongeza kuwa “Rais ameweka wazi kwamba utekelezaji ndiyo kipimo chake, na anatarajia matokeo ya haraka.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *