Rais Volodymyr Zelensky aliwasili Jumatatu nchini Uingereza kwenye ofisi ya Waziri Mkuu Keir Starmer kwenye Mtaa wa Downing namba 10 kwa  ajili ya mazungumzo na washirika wake wa Ulaya kuhusu makubaliano ya amani yaliyopendekezwa na Marekani.

Zelensky alikutana Jumatatu Jioni mjini London na viongozi wa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ili kujadili mpango wa amani uliopendekezwa na Marekani na unaolenga kukomesha  vita kati ya Ukraine na Urusi , mkutano uliokuwa pia wa kudhihirisha uungwaji mkono wa Ulaya kwa Kiev baada ya rais wa Marekani Donald Trump kumshambuli Zelensky kuwa hakuusoma kwa kina mpango huo wa amani.

London 2025 | Starmer na Zelensky wakizungumza kuhusu vita vya Ukraine
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akiwa kwenye mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer mjini LondonPicha: Ben Stansall/AFP

Zelensky alifanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, na baadaye alielekea mjini Brussels-Ubelgiji ili kuendeleza mazungumzo na viongozi wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Kujihami ya NATO, kabla ya kuelekea jana usiku nchini Italia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kufuatia mkutano huo wa London , Zelensky amesema Ukraine haina haki ya kisheria au kimaadili ya kuikabidhi ardhi yake kwa Urusi chini ya makubaliano yoyote yenye lengo la kukomesha uvamizi wa karibu miaka minne.

“Je, tunafikiria kuachia eneo lolote? Hatuna haki ya kisheria ya kufanya hivyo. Kulingana na sheria ya Ukraine, katiba yetu na hata sheria ya kimataifa, hatuna haki ya kimaadili ya kufanya hivyo. Urusi inasisitiza kwamba tuachia baadhi ya maeneo yetu, lakini hakika hatutaki kuachia chochote. Hilo ndilo tunalopigania, kama mnavojua. “

Msukumo wa Marekani kwa mpango huo

Washington D.C. 2025 | Trump akiwa na Zelensky katika Ikulu ya White House
Rais wa Marekani Donald Trump (nyuma) akiwa na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky mjini WashingtonPicha: Ukraine Presidency/Bestimage/IMAGO

Rais Zelensky amesema Marekani ilikuwa ikijaribu bila mafanikio kwa sasa kupatia mwafaka suala hilo la kuachia ardhi, lakini akasisitiza kuwa hawana nia ya kuachilia chochote na ndio maana wanaendelea kupambana na Moscow. Mazungumzo kati ya maafisa wa Marekani na wale wa Ukraine yanaendelea huko Florida- lakini Ikulu ya Kremlin imesema hadi sasa haijafahamishwa matokeo yoyote ya mazungumzo hayo.

Chanzo kimoja kilicho karibu na mazungumzo hayo kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba masuala yanayotatiza kukamilisha mpango huo wa amani ni suala la Ukraine kuachia eneo lake pamoja na hakikisho la usalama, kwa kuwa Kiev inahitaji kufahamu hatua zitakazochukuliwa na washirika wake iwapo Urusi itaanzisha uchokozi mwingine baada ya makubaliano hayo, jambo ambalo Zelensky amesema hadi sasa halijapatiwa jawabu.

Zelensky amesema maafisa wa Ukraine na Ulaya wanaendelea kuufanyia kazi mpango huo uliopendekezwa na Marekani na wenye vipengee 20 kwa sasa na kwamba wanatarajia kufikia leo jioni kuwasilisha kwa Washington mapendekezo yao ya kuboresha mpango huo wa amani.

(Vyanzo: Mashirika)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *