
Hayo yamesemwa Jumanne na Omar Touray, rais wa Tume ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ECOWAS alipokuwa akizungumza na baraza la upatanishi na usalama la jumuiya hiyo ya Kikanda, akiongeza kuwa matukio ya wiki chache zilizopita yameonesha umuhimu wa kutathmini kwa makini kuhusu mustakabali wa demokrasia na hitaji la haraka la kuwekeza katika usalama wa watu wa eneo hilo ambao amesema wako katika hali ya hatari.
Kauli ya Touray imetolea ikiwa ni siku chache tangu kutokea kwa jaribio la mapinduzi nchini Benin, katika mfululizo wa matukio ya mapinduzi ya kijeshi na majaribio ya kuchukua madaraka kimabavu. Jumuiya ya ECOWAS imekuwa ikikabiliwa na ukosoaji kutokana na hatua zake zisizo za uadilifu kwa mapinduzi yaliyoshuhudiwa katika miaka ya hivi karibuni.