
KESHO ni vita katika mchezo wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kati ya timu ya Veins BC na Dar Kings.
Mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam utafanyika kwenye Uwanja wa Don Bosco, Upanga.
Akiongea na Mwanasposti kwenye viwanja vya Spide, kocha wa timu ya Veins BC, Amin Mkosa amesema licha ya mchezo huo kuwa mgumu, timu yake imejipanga vema kuivuruga timu hiyo.
Kwa mujibu wa Mkosa, baada ya timu yake kushinda michezo mitatu mfululizo, wachezaji wake wameahidi kuendeleza moto huo huo.
Timu ya Veins BC katika michezo yake iliyocheza ilishinda timu ya Cavaliers kwa pointi 78–5, Kigamboni Heroes kwa pointi 70–43 na Kigamboni Kings kwa pointi 53–54.
Naye Kamishna wa Ufundi na Mashindano ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Shabani Mahobonya amesema ligi hiyo ilisimamishwa kupisha Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL) iliyofanyika mkoani Dodoma.
Amesema mchezo mwingine unaotarajiwa kufanyika kesho ni kati ya timu za Magone na Leaders, Mlimani BBC na Kigamboni Kings, PTW na KR 1.
Timu zinazoshiriki ligi hiyo ni Game Time Squad, Ukonga Kings, Kigamboni Heroes, Cavs, Crows, Veins BC, Leaders, Primer Project Academy na Magone.
Timu nyingine ni Kigamboni Basketball Club, Leo Kings, Yellow Jacket, Ukonga Warriors, Mlimani, Kibada Riders, Basketball Club, Dar Kings, DB VTC na Mbezi Beach Spurs.
Ligi hiyo ya daraja la kwanza mkoa wa Dar es Salaam inafanyika kwa lengo la kutoa timu tatu zitakazoshiriki Ligi ya BDL mwakani.
Katika ligi iliyofanyika mwaka jana, timu ya Polisi, Stein Warriors na Kurasini Heat ndizo zilizopanda daraja.