SEHEMU ya kwanza katika mfululizo wa makala hizi zilizotokana na mahojiano maalumu na kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa sasa Wydad Casablanca, Stephanie Aziz KI, tuliona namna jamaa alivyotua Morocco na kumpiga biti kocha Mohamed Benhachem ili kuingia kikosi cha kwanza.

Pili aliweka bayana namna alivyoshindwa kuelewa kilichoendelea baada ya kugongana uwanjani na Himid Mao na kuanguka katika pambano la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Azam na kueleza namna maisha yake Wydad yalivyo licha ya ugumu wa awali wa kuiacha Yanga.

Leo tunaendelea sehemu ya pili ya mahojiano hayo na nyota huyo raia wa Burkina Faso amefunguka mambo mengine zaidi hususan yalivyokuwa maisha yake Yanga na jinsi alivyokuja kumuoa Hamisa Mabetto, aliyedai awali haikuwa rahisi kwake. Ki vipi? Endelea naye…!

UAMUZI YA KUMUOA HAMISA

Aziz KI anaanza kwa kueleza namna alivyopiga hesabu zake na kumpata Mobeto anaanza hivi:

“Nikiwa mkweli kwako kwanza nilikuwa na furaha, lakini nina uhakika asilimia 90 za watu hawamjui vizuri mke wangu (Hamisa Mobeto), hawajui namna ni mkarimu kiasi gani na mtu ambaye ananisapoti, hata mimi wakati naanza naye nilishtuka sana. Nakumbuka wakati tunaanza mahusiano sikujua kama huyu ndiye Hamisa wa ndani ninayemjua kwa nje, wakati tunaanza kuongea.

“Ni mtu tofauti na huyu mnayemwona nje, akiwa nyumbani ni mama wa familia, anajali sana ni mtu mzuri ni mcha Mungu, kwangu mimi ilikuwa ni maamuzi sahihi kumuoa, ilikuwa rahisi kwa kuwa alinionyesha na nikajiridhisha ni mtu sahihi namshukuru Mungu na nina mpenda sana.”

ILIKUWA RAHISI KUMUOA?

“Ilikuwa rahisi kwa kuwa alifanya kila kitu kuwa rahisi kwangu, ni mtu ambaye alibadilisha maisha yangu. Kuna namna yamekuwa ya furaha zaidi tangu tumekuwa pamoja, naweza kusema kabla ya kuoa alinifanya nijione nimekua na nina maisha mazuri na yenye furaha.”

HAMISA AMWEKEA BONASI

Kama hufahamu basi chukua hii. Aziz KI kwake bonasi kwa sasa siyo ile tu anayoipata kwenye timu yake, kuna nyingine inaanzia nyumbani akiwekewa malengo na mke wake Hamisa na  kila anapoingia kwenye mechi kuna bonasi anatakiwa kuiwania kutoka kwa mkewe huyo.

“Ananisapoti katika kila kitu kuhusu kazi yangu, kuanzia ratiba yangu ya mazoezi mpaka kwenye mechi, mfano nataka kukwambia kuanzia wakati nikiwa hapa, alikuwa kila mechi ananipangia bonasi ambayo ili niipate natakiwa kufikia malengo anayonipa, kama leo nikishinda kwa kufunga utapata hii zawadi au ukitoa asisti utapata hiki.

“Nikiitimiza naipata kweli baada ya mechi, kwangu hii ilikuwa changamoto nzuri ambayo ilinifanya nijitume sana ili niipate, kwangu mimi thamani haikuwa kile anachonipatia ilikuwa ni namna mtu uliye naye anajali kuona unafanikiwa kwenye kazi yako, ilikuwa inanipa hamasa ya kuhakikisha nafanya vizuri na kuwa bora.”

AKIKOSA HAPATI KITU

“Ni kweli kama nikishindwa kufikia malengo alikuwa hanipi kitu, huwa hapendi kuona nacheza mechi halafu inamalizika bila ya mimi kufunga alikuwa anachukia sana, anapenda niwe nafunga kila mchezo, naweza kurudi nikawa sijafunga na namwambia nimecheza vizuri ila sijafunga, ataniambia hapana kwake kucheza vizuri ni kufunga bao au mabao, kuna wakati namwelewesha mimi ni kiungo jukumu langu ni kutengeneza nafasi anasema sawa lakini anataka ufunge, hayo mengine hataki kusikia anasema mimi ni Master KI, naichukulia mrengo chanya ni kama morali kwangu.”

AKIPOTEZA MECHI ANAMFARIJI

“Ikitokea tumepoteza mchezo, ni mtu mwema pia atahakikisha natoka kwenye masikitiko, atazungumza na mimi vizuri, ataniombea dua kwa Mungu, ananiambia Mungu hawezi kukupa unachotaka kila wakati, chochote unachopata mshukuru Mungu, kuna wakati niwe na subira, duniani kuna kupanda na kushuka, atasema najua leo umepoteza lakini kesho hakikisha haupotezi tena.”

WANAWASILIANA MARA NGAPI KWA SIKU?

“Mimi nalala na mke wangu kwenye simu, unajua Hamisa ni rafiki yangu mkubwa wa kwanza kwa hiyo suala siyo tunawasiliana mara ngapi, kabla ya kwenda mazoezini lazima tuongee, kabla ya kwenda kwenye mechi tutaongea, nikiwa nakwenda kula nitamtumia picha ya chakula ninachokula siku husika.

“Tunawasiliana sana kila wakati na kila tukio, hata kama tukiwa mbali najiona kama niko naye wakati wote hata nikiwa nataka kwenda kwenye mazoezi au mechi ataniombea dua au atanitumia sura ya dua niisome kabla ya kuanza kazi, nikitaka kulala pia tunamshukuru Mungu.”

MAPENZI YA MBALI ANAMUDU VIPI?

“Kwanza lazima watu wafahamu ndoa siyo kama utani, hamtakiwi kuangalia kuhusu watu wanasema nini juu yenu.

“Ndoa ni namna mnavyoamua kukubaliana kuwa pamoja na kupeana sapoti, kabla ya kumuoa nilijua  mke wangu ni mtu maarufu na ana shughuli zake za kazi, sasa siwezi kumuona kisha nikamwambia unatakiwa kuacha hii kazi na unifuate ninapokwenda.

“Kwa kiwango kilekile anavyonisapoti kwenye kazi yangu, anakuja uwanjani kutazama mechi na mimi kwa kiwango kilekile natakiwa kuhakikisha namsapoti kwenye majukumu yake, namuombea na kumsaidia awe mkubwa na anayejulikana zaidi, aweze kupata nafasi mbalimbali, maisha yetu hayapo kwa mrengo wa kujionyesha, kitu muhimu nataka kuona mke wangu ana furaha, tunawezaje kuwa sawa na familia zetu na muhimu baada ya majukumu yetu tunakuwa pamoja kama familia na kufurahia.

“Kwetu ni kitu rahisi kwa sababu muhimu ni furaha yetu wawili, kwa hiyo watu wanasema nini siwezi kukipeleka kwa mke wangu wala yeye kuleta kwangu.”

HAWAGOMBANI?

“Hapana hatujawahi kugombana kama nilivyokwambia tulishajuana kabla kila mmoja na majukumu yake kuna wakati nakwenda kucheza mbali mke wangu anaelewa sana kwa kuwa tunapata wakati wa kuzungumza.

“Hawezi kuniambia hataki niende kwa kuwa hii ni kazi, pia mimi najua kazi za mwenzangu kuna wakati anatakiwa kukutana na watu kwa kazi zake, nampa nafasi ya kufanya hivyo kwa kuwa najali majukumu yake. Hatujawahi kutofautiana hata kama yupo hapa na mimi nikiwa mbali, unajua hata wakati nahamia Wydad alikuwa anajua na tulishazungumza na akaelewa.”

HAKUNA WIVU WA KIJINGA

“Unajua unatakiwa kuelewa kitu, kabla ya kuoa au kuolewa na mtu unatakiwa kujua natakiwa kumwamini mke wangu kwa asilimia mia moja kama ambavyo mimi namwamini.

“Kabla ya kumuoa nilikuwa najua ni modo, unajua hata sisi wachezaji tunasafiri maeneo tofauti na tukakutana na watu tofauti lakini unaona wala halalamiki kwa hiyo na mimi sitakiwi kulalamika.”

DABI YA WYDAD, RAJA YAMSHTUA

Aziz KI mara baada ya kujiunga na Wydad alicheza dabi yake ya kwanza Oktoba 29,2025, walipoikaribisha Raja Athletic uliomalizika kwa sare isiyo na mabao, anasimulia namna alivyoshangaa akiita dabi kubwa duniani.

“Ilikuwa kama kichaa hivi, kwangu mimi hii ni dabi kubwa duniani, nilikuwa na furaha kwa kupata uzoefu kucheza mchezo mkubwa kama ule, ni mchezo tofauti kabisa wa dabi kama huu mnauona hapa Tanzania, presha ni kubwa kwa timu zote lakini ukiwa mchezaji hutakiwi kuibeba hiyo, unatakiwa kuiacha kwa mashabiki na viongozi. Bahati mbaya hakutukushinda lakini tulicheza vizuri, ulikuwa mchezo mzuri.”

FADLU ASHUKURU KUTOLEWA

Wakati Aziz KI anacheza Wydad kwenye dabi, alikutana na Kocha Fadlu Davids ambaye anaifundisha Raja akitokea Simba na anasimulia walivyokutana.

“Alifurahia nilipotolewa (Fadlu), aliniambia nilishukuru kocha wako alipokutoa, alikuwa na wasiwasi na mimi kwa sababu ananijua vizuri, ukweli ni kwamba nina heshima kubwa sana na Fadlu ni kocha mzuri sana, amefanya makubwa msimu uliopita alipokuwa Simba.

“Mpaka tunakutana naye alikuwa na wiki moja tu lakini alibadilisha mambo mengi pale (Raja), nilifurahia kumuona amerejea Morocco.”

ATARUDI BONGO?

“Huwezi kujua hii ni soka huwezi kusema hapana, huwezi kusema ndiyo, lakini mimi siku zote naiacha kesho iwe ya Mungu, kama nafasi inakuja kwa nini usiichukue, kama unaona kuna kitu kizuri unaweza kukipata.

“Unafanya maamuzi kwa ajili yako na familia, kwa sababu kila kitu unachofanya siyo kwa ajili yako peke yako na familia pia.”

YEYE NI MUVI, KUPIKA

“Nikiwa kwenye mapumziko nje ya kazi yangu napenda sana kuangalia muvi, kucheza playstastion na kupika, napenda sana nikiwa nyumbani nasaidiana na mke wangu kuwapikia watoto.

“Bahati mbaya siwezi kupika vyakula vya Kitanzania lakini namsaidia vitu mke wangu na anajua sana kupika, naweza kupika nyakula ambavyo hapa Tanzania hamvijui kama atekee, pasoo hivi ni vyakula kwa kule kwetu.”

HATAKI UGALI

“Mimi napenda sana pilau, ndiyo chakula changu pendwa, makange ya samaki napenda sana, chapati, chipsi mayai, hivyo ndivyo vyakula ambavyo hapa Tanzania navipenda sana, lakini ugali hapana sipendi wala wali sio mpenzi sana, unajua mimi sio mtu mlaji sana na bahati mbaya sipendi kula chakula ambacho sikifahamu lakini namshukuru mke wangu anaendelea kunibadilisha taratibu.”

“Namshukuru Mungu nina mke ambaye anaelewa ni mambo gani natakiwa kuzingatia wakati wa vyakula, unajua maisha yetu muda mrefu tunakuwa kambini, ni siku chache sana tunakuwa nyumbani.

“Lakini mke wangu anazingatia sana vyakula ambavyo sitakiwi kuvitumia sana ili nisiongeze uzito wa mwili na wakati mwingine namsaidia kumwelewesha hiki sitakiwi kufanya sasa wala kukitumia na anaelewa.”

Itaendelea Jumatatu

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *