WAKATI Mwanaspoti likiendelea kukuhabarisha mchakato mzima wa kocha mpya wa Simba unavyofanyika, kuna sababu tatu zimetajwa zinazombeba Mtuinisia, Mohamed Sahli.
Kocha huyo ambaye Mwanaspoti linafahamu amefikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na viongozi wa Simba katika kupewa jukumu la kuiongoza timu hiyo, anabebwa na uzoefu wake wa soka la Ukanda wa Afrika Kaskazini akiwa amezaliwa huko na kufundisha, pia mbinu bora za ushindi na malengo ya klabu hiyo.
MCHAKATO ULIVYOANZA
Katika kumsaka kocha mpya Simba, mchakato ulianza mara tu klabu hiyo ilipotangaza kusitisha mkataba na Dimitar Pantev, Desemba 2, mwaka huu, kisha kikosi hicho kuwa chini ya Seleman Matola ambaye baadaye alipigiwa chapuo kupewa timu moja kwa moja, lakini kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Azam, kilitibua kila kitu.
Hata hivyo, Matola ambaye alikuwa akipigwa presha ya kutakiwa kuondoka Simba, viongozi wa klabu hiyo wamekubaliana abaki, huku kocha mkuu mpya anayekuja, afanye naye kazi sambamba na wasaidizi wengine.
Kabla ya Simba kubaki na Sahli hivi sasa, makocha kibao walituma wasifu wao kuomba kazi ndani ya klabu hiyo, huku jina la Antonio Casano Cantos kutoka Hispania akiwa na sifa za kufundisha soka Angola na Morocco kupitia timu za Petro Atletico na Moghreb Atletico Tetouan likipenya hatua za mwisho za mchujo. Mwingine ni kocha wa Stellenbosch, Steve Barker raia wa Afrika Kusini.
Hata hivyo, taarifa zaidi zilizolifikia Mwanaspoti ni, mchakato wa kumsaka mrithi wa kuziba nafasi ya Pantev umesukiwa mikakati tofauti ikiwamo katika kikao ambacho mabosi wa Simba walikutana wiki hii kutoka upande wa Mwekezaji Mohammed ‘MO’ Dewji na wale wa klabu chini ya Mwenyekiti Murtaza Mangungu.
Taarifa hizo kutoka Simba, zilibainisha kikao hicho kilichokutanisha pande hizo mbili, kulikuwa na makubaliano ya kuweka majina ya makocha waliotuma maombi, kisha mchujo kufanyika na kubaki majina matatu ambayo yamefanyiwa uchunguzi wa kina ili kuondoka na jina moja.
HALI ILIVYO SASA
Mwanaspoti linafahamu, Simba hasa upande wa bodi ya wakurugenzi imemtafuta kocha Mtunisia, Mohamed Sahli, ambaye tayari amepokea simu ya Wekundu hao wa Msimbazi wakitaka kujua utayari wake wa kuifundisha timu hiyo na masilahi kwa jumla.
Sahli ambaye amewahi kuifundisha US Monastir ya Tunisia, kwa sasa hana timu tangu Julai 22, 2025 alipoachana na Club Africain ya hukohuko Tunisia.
Hesabu za Simba ni mbali na ubora wa Sahli kimbinu, lakini wanataka akili yake watakapokutana na Esperance de Tunis kwenye mechi ya tatu ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika iwe rahisi kuwachapa Watunisia hao na kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali.
MIPANGO YA WEKUNDU
Taarifa za ndani zimeliambia Mwanaspoti: “Tunataka kocha mzuri kimbinu lakini anayeweza kutuvusha salama kwenye hizi mechi mbili zijazo za CAF dhidi ya Esperance. Hizi ni mechi ambazo heshima yetu ipo hapo, hatuwezi kukubali kupoteza pointi kirahisi na haituingii akili kuona Simba inaishia makundi msimu huu.
“Kama tukikubaliana, atakuja huyu Sahli haraka ili aanze mikakati mapema kipindi hiki ligi imesimama na asuke kikosi chetu haraka kabla ya Januari kuanza mechi hizo za CAF.”
Mtoa taarifa huyo aliendelea kubainisha, endapo ikishindikana kwa Sahli, basi Simba itaendelea kupiga kambi ukanda huohuo wa Kaskazini mwa Afrika kusaka kocha mwingine kwa sababu moja kuu ikitaka kutafuta mtu atakayewabeba mbele ya Waarabu hao watakaokutana nao Januari 23 na 30 mwaka 2026.
KOCHA WA AINA GANI?
Sahli aliyezaliwa Tunisia Machi 24, 1978 akiwa pia na uraia wa Austria, ana Leseni ya UEFA Pro, huku akipendelea mfumo wa 4-3-3. Umri wake kwa sasa ni miaka 47.
Sahli amekuwa mkufunzi wa vijana ndani ya ASV Blau-Weiss Salzburg tangu mwaka 2008, ambapo pia alikuwa akifanya kazi kama mchezaji wakati huo.
Kuanzia Machi 2009, alifundisha timu za vijana za Salzburger SK 1919. Kwa msimu wa 2008-09, alijiunga na Red Bull Salzburg.
Kati ya 2012 na 2013, alifundisha timu za vijana za timu ya akiba ya FC Liefering, kabla ya kurejea Salzburg.
Msimu wa 2015-16, alikuwa mkufunzi wa timu ya akiba ya SV Grödig iliyokuwa ikishiriki Ligi Daraja la Nne na kumaliza nafasi ya tatu, lakini akajiondoa kutokana na timu ya kwanza kushuka daraja kutoka Ligi Kuu.
Alipoondoka hapo, Sahli akawa kocha wa vijana SK Sturm Graz kwa msimu wa 2016-2017. Kuanzia 2017, pia aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya Austria chini ya miaka 19.
Baada ya msimu wa 2017–2018, aliondoka Sturm Graz kwa sababu za kifamilia. Kuanzia 2018, alikuwa kocha msaidizi wa Martin Scherb na timu ya Austria chini ya miaka 16.
Kwa msimu wa 2019-2020, alijiunga na Wolfsberger AC katika Ligi Kuu Austria na kuwa kocha msaidizi wa Gerhard Struber. Kufuatia kuondoka kwa Struber aliyetimkia FC Barnsley Novemba 2019, Sahli akawa kocha mkuu wa muda klabuni hapo.
Desemba 2019, nafasi yake ikachukuliwa na Ferdinand Feldhofer.
Julai 8, 2024, alitangazwa kuwa Kocha Mkuu wa US Monastir ya Tunisia, akirithi nafasi ya Lassaad Chabbi. Hata hivyo, hakudumu sana kwani Mei Mosi, 2025, akatua Club Africain kama mkurugenzi wa michezo na mshauri wa kiufundi.
Kabla ya hapo, Sahli alikuwa amekataa ofa kutoka Shirikisho la Soka la Tunisia.
Rekodi zinaonyesha nafasi hiyo aliitumikia hadi Julai Mosi 2025 alipopewa jukumu la kuwa kocha mkuu na kuachana na timu hiyo Julai 22, 2025. Kwa sasa timu hiyo inanolewa na Faouzi Benzarti.
KUHUSU MSAIDIZI WAKE
Simba itaendelea kusalia na Matola kama kocha msaidizi, huku atakayeteuliwa kuwa Kocha Mkuu hata kama akija na wasaidizi wake, haitaathiri chochote uwepo wa mzawa huyo ambaye amefanya kazi na makocha tisa wa kigeni tangu 2019 alipotua akitokea Polisi Tanzania.
MTIHANI ULIPO
Baada ya Simba kupoteza mechi mbili za Kundi D katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu dhidi ya Petro Atletico (1-0) na Stade Malien (2-1), timu hiyo inatakiwa kuifunga Esperance katika mechi mbili zijazo zitakazochezwa Januari 23, 2026 nchini Tunisia, kisha kurudiana Januari 30, 2026 jijini Dar ili kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali kutokana na hivi sasa haina pointi.
WIKI TATU ZATENGWA
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kutakuwa na takribani wiki tatu hadi nne za kocha huyo mpya kusuka kikosi kazi kwa ajili ya kuanza kukusanya pointi katika michuano ya CAF itakapoendelea Januari 2026.
Ally alisema kwa sasa kikosi hicho kipo kwenye mapumziko mafupi baada ya Desemba 7, 2025 kumalizana na Azam katika mechi ya Ligi Kuu Bara ambayo ilipoteza kwa mabao 2-0.
“Tutakaporejea kuendelea na maandalizi ya mechi zetu kuanzia Januari 23 mwakani tunataka tuwe tushapata kocha tayari. Yaani tumpe mwalimu kama pre-seasom fulani hivi ya wiki tatu au nne ili awajue wachezaji. Tutakapoanza mechi za mashindano awe tayari familia na kikosi chake.”