
Uhasama kati ya Thailand na Cambodia umeendelea siku ya Jumamosi, Desemba 13, huku Phnom Penh ikiishutumu jeshi la Thailand kwa kufanya mashambulizi ya anga katika eneo lake. Bangkok imethibitisha operesheni zaidi za kijeshi licha ya tangazo la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba nchi hizo mbili zimekubaliana kusitisha mapigano.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Thailand itaendelea kufanya vitendo vya kijeshi hadi tutakapoiona nchi yetu na watu wetu hawatishiwi tena,” Waziri Mkuu wa Thailand Anutin Charnvirakul amesema kwenye Facebook. Jeshi la Thailand lilithibitisha “mashambulizi ya kulipiza kisasi” dhidi ya malengo ya Cambodia mapema Jumamosi asubuhi. Wizara ya Ulinzi ya Cambodia, kwa upande wake, inadai kwamba ndege mbili za kivita za Falcon za Thailand F-16A/B zilidondosha mabomu saba katika maeneo kadhaa. Kwa kujibu, Cambodia imetangaza kufungwa kwa vivuko vyote vya mpaka na jirani yake. Kulingana na Wizara ya Ulinzi ya Thailand, ikinukuliwa na hirika la habari la AFP, wanajeshi wake wanne waliuawa mpakani, na kufikisha jumla ya majeruhi kumi na wanne wa Thailand tangu mapigano yalipoanza tena siku ya Jumatatu.
Kwa miongo kadhaa, nchi hizo mbili zinapigana kuhusu maeneo ya mpaka, ikiwa ni pamoja na hekalu la Preah Vihear.
“Eneo hili ni muhimu kwa sababu ni la kidini na kwa hivyo lina ishara kali sana ya uzalendo. Ubuddha ni dini ya serikali nchini Thailand, na ni wazi kwamba hata mfalme amejitolea kulinda mahekalu. Kwa hivyo, kuna hisia kali ya utambulisho inayodaiwa na nchi zote mbili, ambayo huipa hekalu hili thamani fulani”, amesema Sophie Boisseau du Rocher, mtaalamu wa masuala ya kijiografia huko Asia.
Mapigano haya mapya yanakuja baada ya wiki moja ya vurugu kando ya mpaka wa pamoja, ambayo ymesababisha vifo vya watu wasiopungua ishirini na kusababisha mamia ya maelfu ya raia kukimbia pande zote mbili. Saa chache mapema, Donald Trump alidai kwamba Bangkok na Phnom Penh zimekubaliana kusitisha uhasama na kurudi kwenye makubaliano ya awali ya amani yaliyosimamiwa mwishoni mwa mwezi Oktoba chini ya usimamizi wake, kwa usaidizi wa Malaysia. Hata hivyo, hakuna upande uliothibitisha makubaliano haya ya amani, kulingana na mwandishi wetu huko Bangkok, Valentin Cebron.
“Nilikuwa na mazungumzo mazuri asubuhi ya leo na Waziri Mkuu wa Thailand, Anutin Charnvirakul, na Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Manet, kuhusu kuibuka tena kwa kusikitisha kwa vita vyao vya muda mrefu. Wamekubaliana KUKOMESHA mapigano yote kuanzia usiku wa leo na kurudi kwenye makubaliano ya awali ya amani yaliyofikiwa nami na wao, kwa msaada wa Waziri Mkuu mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim,” rais wa Marekani aliandika siku ya Ijumaa jioni kwenye mtandao wake wa Truth Social. “Nchi zote mbili ziko tayari kwa AMANI na kuanza tena kwa biashara na Marekani,” Donald Trump aliongeza.