Wazee wa Baraza la Mila na Desturi mkoani Ruvuma wameamua kufunga mvua kwa siku zote zitakazokuwa zinaendelea shughuli za mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mhe Jenista Mhagama, kama ishara ya heshima, majonzi na kutambua mchango wake mkubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu Mhe Jenista Mhagama, Katibu Mkuu wa Baraza la Mila na Desturi mkoa wa Ruvuma, Chifu Abbas Mpumule Chitete, amesema kuwa baraza hilo ndilo lililomsimika Mhe Jenista Mhagama kuwa “Malkia wa Jimbo la Peramiho” katika kijiji cha Mpitimbi.

Amesema hatua hiyo ilitokana na ukaribu wake mkubwa na baraza la mila na desturi pamoja na mchango wake wa dhati katika kulinda, kuthamini na kuendeleza mila na desturi za jamii ya Ruvuma.

Chifu Chitete ameongeza kuwa marehemu alikuwa na uhusiano wa karibu sana na baraza hilo, huku akieleza kuwa baba mzazi wa Mhe Jenista Mhagama aliwahi kuwa mweka hazina wa Baraza la Mila na Desturi mkoa wa Ruvuma, jambo lililoendelea kuimarisha mshikamano wao na familia ya marehemu.

Aidha, imeelezwa kuwa Mhe Jenista Mhagama alizaliwa siku ambayo kulikuwa na mvua kubwa, na hata siku ya kufariki kwake kumeshuhudiwa kunyesha kwa mvua, jambo ambalo kwa mujibu wa mila na desturi lina tafsiri na alama maalum.

Kutokana na hilo pamoja na mchango wake mkubwa katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Peramiho, mkoa wa Ruvuma na taifa kwa ujumla, Baraza la Mila na Desturi mkoa wa Ruvuma limeamua kuifunga mvua hadi pale shughuli zote za mazishi ya Mhe Jenista Mhagama zitakapokamilika.

#CloudsDigitalUpdates

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *